Saturday, 27 February 2016

MAGUFULI ANAMTOA MACHOZI NYERERE KABURINI!



NA LUQMAN MALOTO
VEMA kuitambua na kuiheshimu misingi iliyoasisi taifa letu. Kwamba pamoja mambo mengi, katika Kitabu cha Azimio la Arusha, sehemu ya madhumuni ya Tanu, kipengele (b), ni kuhusu msimamo wa nchi kwa haki za binadamu.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwaongoza waasisi wa taifa hili kuishi misingi yake na kusimama kidete juu ya uvunjwaji wa haki za binadamu popote pale ulipokuwepo.
Katika madhumuni hayo ya Tanu, Azimio la Arusha toleo la mwaka 1967, kipengele (d), kinasomeka: “Kushirikiana na vyama vyote vya siasa katika Afrika, vinavyopigania uhuru wa bara lote la Afrika.”
Na katika kusimamia hilo, historia ya Bara la Afrika, inamtambulisha Mwalimu Nyerere kama askari shupavu aliyesimamia vuguvugu la ukombozi wa nchi zake, hususan zile za Kusini ya Jangwa la Sahara.
Hivi karibuni, Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, alizindua kitabu alichokiandika na kukipa jina “Mwalimu Julius Nyerere Asante Sana”, ndani yake akieleza jinsi ambavyo alisimama imara kuhakikisha Afrika inakuwa huru.
Kitabu hicho ni heshima kwa mchango wa Mwalimu Nyerere ambaye baada ya Tanganyika kupata uhuru hakupumzika na kutawala nchi yake kwa nafasi, badala yake alielekeza nguvu zake za kifikra, kifalsafa hata kirasilimali ili kulikomboa bara zima kisha kuasisi wazo la kuunda Umoja wa Afrika.
Rejea ya Mwalimu Nyerere na Umoja wa Afrika, inakumbusha hata nukuu yake wakati wa kuuwasha Mwenge wa Uhuru na kuupandisha kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, aliposema: “Sisi watu wa Tanganyika, tunapenda kuwasha Mwenge juu kabisa ya kilele cha Mlima Kilimanjaro.
“Mwenge ambao utamulika mpaka nje ya mipaka yetu, upeleke amani pasipo na amani, upendo penye chuki, matumaini kwa waliokata tamaa, utu pasipo na utu.
“Hatuwezi, tofauti na mataifa mengine, kupeleka roketi mwezini, lakini tunaweza kutuma roketi za upendo na matumaini kwa ndugu zetu, popote walipo.”
Rejea hizo, zinaonesha kuwa mara tu Tanganyika ilipopata uhuru, makali ya kwanza ya Mwalimu Nyerere yalikuwa kuikataa Afrika Kusini ya Kikaburu ndani ya Jumuiya ya Madola (Commonwealth), kwa maelezo kuwa siyo sawa kushirikiana na nchi inayokandamiza na kutesa raia wake bila huruma.
Mwalimu Nyerere alisema: “Tunaamini kuwa uanachama wa Afrika Kusini chini ya hali halisi iliyopo sasa, unaleta utani wa ushirikiano wetu kwenye Jumuiya ya Madola.
“Hatuwezi kujiunga na umoja wowote wa kirafiki ambao unajumuisha dola ambayo kwa makusudi na bila huruma inawanyanyasa raia wake kwa misingi ya ubaguzi wa rangi.”
Vilevile, Desemba 5, 1965, Mwalimu Nyerere alitishia kuvunja uhusiano wa kibalozi na Uingereza, kutokana na vitendo vya ukosefu wa utu ambavyo nchi hiyo ilikuwa ikivifanya dhidi ya Rhodesia ya Kusini (Zimbabwe), kipindi hicho taifa hilo lilikuwa halijapata uhuru wake.
Msimamo huo wa Mwalimu Nyerere, ulienda pamoja na kufanya mazungumzo na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Arthur Bottomley kisha kumweleza kuhusu dhamira ya Tanzania kujitoa kwenye umoja huo wa Commonwealth.
Hiyo ndiyo misingi iliyoasisi taifa letu. Siku zote tumekuwa pamoja na wanyonge wenye kukandamizwa. Hatufungamani na wanyonyoji au wakandamizaji, achilia mbali mabeberu.
Na hii ndiyo sababu kwamba Mwalimu Nyerere ni mkubwa mno barani Afrika kuliko hata marehemu Nelson Mandela. Mwalimu aliwekeza katika kuhakikisha Afrika inakuwa huru.
Maono ya Mwalimu Nyerere tangu mwanzoni mwaka miaka ya 1960 yalikuwa kufanikisha Umoja wa Afrika. Kitabu cha Azimio la Arusha, kinaonesha maono haya. Kimsingi falsafa za Mwalimu Nyerere zina thamani kubwa mno.
Hii ndiyo sababu Mugabe aliwahi kuwakejeli wenye kumtukuza sana Mandela kuliko Nyerere, akawaambia: “Mandela alipigania nchi yake pekee, Nyerere alipigania bara zima la Afrika.”
Unaweza kujiuliza ni kwa nini Tanzania ilifungamana na Cuba, yenye uhasama na Marekani? Au mataifa mengine madogomadogo yaliyokuwa yakikandamizwa na mabeberu?
Na hii ndiyo ikawa sababu ya Tanzania kutokuwa na ushirikiano wa kibalozi na Israel. Ni kwamba Waisrael wanawanyanyasa Wapalestina. Na msimamo wetu kama taifa ni kushirikiana na wanyonge ili ikiwezekana kuwasaidia kuutokomeza unyonge dhidi yao.
Tanzania haikuwahi kuwa na ushirikiano wa kidiplomasia na Israel si kwa bahati mbaya. Ulikuwa uamuzi mahsusi kuonesha kutopendezwa na mgogoro wa Mashariki ya Kati.
Unaweza kujiuliza ni kwa nini ubalozi wa Palestina umekuwepo nchini miaka mingi iliyopita lakini Israel haukuwepo? Unadhani Waisrael ndiyo hawakuwa na mpango? La hasha! Mwalimu Nyerere aliwakatalia.
Ni msimamo huo ambao uliheshimiwa na Rais wa Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, ukaendelewa na Rais wa Tatu, Benjamin William Mkapa kisha ukadumishwa na Rais wa Nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
Ni kwa nini leo Tanzania chini ya Rais wa Tano, Dk. John Pombe Magufuli, nchi imeingia makubaliano ya kibalozi na Israel? Marais waliopita wao ndiyo walikuwa wanakosea au Dk. Magufuli?
Je, tumeanza kushirikiana na watu wenye kukandamiza wenzao? Sababu zilizoifanya Tanzania kukataa ushirikiano wa kibalozi na Israel, kwa sasa zimeondoka?
Mbona hali ya amani Mashariki ya Kati bado ni tete vilevile? Vigezo vipi ambavyo leo vinaifanya Tanzania isaliti misimamo ya waasisi wa taifa letu? Kipi kinasababisha tuipige teke misingi ya kuwamulikia wenzetu upendo na matumaini?
Hiki ni kipindi ambacho hata mataifa yaliyokuwa kumbatio hasa la Waisrael, kama Marekani, yameanza kutetea mamlaka ya Palestina kama taifa.
Tayari Palestina imeshapewa uanachama wa Umoja wa Matifa. Hii ni hatua muhimu mno kuelekea mamlaka kamili. Ni matokeo mazuri ya misimamo ya akina Mwalimu Nyerere kuupiga vita ukandamizaji wa Israel kwa Palestina.
Ni vigezo gani vimetumika kuikubali Israel kirahisi-rahisi? Je, Dk. Magufuli na timu yake walizingatia msingi wa nchi kukataa ushirikiano wa kibalozi na taifa hilo?
Kwa wenye kuamini kuwa yapo maisha baada ya kifo. Kwamba binadamu huendelea kuishi baada ya kiwiliwili chake kuzikwa kaburini, basi tunamuona Mwalimu Nyerere akitoa machozi mengi kwa uamuzi huo.
Lazima alie, ni matumaini yapi tunayapeleka Palestina kwa kuanzisha ushirikiano na watesaji wao? Machozi ni mengi, ni ujumbe upi ambao leo Tanzania inausambaza kwa ulimwengu?
Matamko ambayo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Bembe alikuwa akiyatoa wakati wa utawala wa Dk. Kikwete, ndiyo hasa yenye kubeba misingi ya waasisi wa taifa hili.
Kama ambavyo ilikuwa wazi kuwa uvamizi wa Marekani, Uingereza na Ufaransa nchini Libya haukukubalika. Ndivyo na nchi ilisimamia. Misingi ya taifa letu ni kila nchi kuheshimu mipaka ya wengine.
Waisrael hawaheshimu wala kutambua uwepo wa Wapalestina, na kwa vile wana nguvu, ndiyo maana wamakuwa wakiwanyanyasa jinsi wanavyotaka. Wapalestina nao kufikisha ujumbe wa chuki dhidi ya ukandamizaji wanaofanyiwa, huamua tu kujitoa muhanga.
Membe chini ya Dk. Kikwete aliwahi kusisitiza jinsi ambavyo mapambano ya Waisrael na Wapalestina yasivyo na ulinganifu, maana Waisrael wanatumia silaha nzito, wakati Wapalestina wanahangaika na mawe. Hawana nguvu hata kidogo.
Kama Tanzania iliwakataa Waisrael kwa kutowaheshimu Wapalestina, je, hivi sasa wanawaheshimu? Iliwakataa kwa kutowatambua, je, sasa wanawatambua? Maswali hayo tu!
Hapa sina maana kuwa kila kilichosimikwa na waasisi wetu lazima kifuatwe kama kilivyo, la hasha! Yapo mambo mengi tu lazima yabadilike kulingana na mahitaji ya wakati. Maono ya miaka 50 iliyopita yanapaswa kuhakikiwa uhai wake kila wakati.
Hili la Israel mpaka sasa uhai wake upo. Maana hawajafanya mabadiliko yoyote. Waisrael hakuna kitu wasichokipenda kama uhuru wa Palestina. Wanataka hawa watu waendelee kuwepokuwepo tu, wawanyanyase na kuwakandamiza wanavyotaka.
Na katika hili ni vema watu wakajifunza siasa za Mashariki ya Kati. Wengi wamekuwa wakilibeba suala la mgogoro wa Mashariki Kati kama uhasama wa kidini.
Watu wanajidanganya kuwa kwa vile inatajwa Israel, basi ndiko kwenye Ukristo, na kwa Wapalestina, vile ni Waarabu, basi ni Uislam.
Wapo Waislam wanaichukia Israel kwa sababu kwamba Wapalestina ni Waislam wenzao. Wanautazama mgogoro huo kwa jicho la kiimani.
Kuna Wakristo hawataki kabisa kuwasikia Wapalestina, kwa sababu mahasimu wao, yaani Waisrael ndiyo Wakristo wenzao. Jicho lao limemezwa na udini tu.
Ukweli ni kuwa mgogoro wa Mashariki ya Kati siyo dini. Na ndani ya Palestina kuna Wakristo wengi ambao wamekuwa wakipata shuluba nzito kutokana na kadhia ya Mashariki ya Kati.
Ni kwamba Waislam na Wakristo wapo pande zote mbili, kwa Palestina na Israel ambako pia kuna Wayahudi ambao siyo Waislam wala Wakristo, wana imani yao na kitabu chao.
Kuweka sawa, ni kuwa kila dini iliyopo Israel na Palestina ni hivyohivyo. Ni tatu, Ukristo, Uislam na Uyahudi. Watu wote pande zote mbili wamegawanyika kiimani katika dini hizo mbili.
Muislam anapowachukia Waisrael kwa sababu za kidini anachekesha, maana Israel kuna Waislam wenzake. Wakristo kutowataka Wapalestina kidini, ni upungufu wa utambuzi, maana wanawakataa Wakristo wenzake.
Wala siyo Uyahudi na Uarabu, maana ndani ya Israel kuna Wayahudi asilimia 74.9, Waarabu asilimia 20.7, na jamii nyingine ni asilimia 4.3. Hii ina maanisha kuwa Israel ni taifa la Wayahudi na Waarabu.
Palestina wao wanajiita Wapalestina lakini ni jamii kubwa ya Waarabu na Wayahudi. Na ndiyo maana zipo jamii za Kipalestina na Israel zinafanana kabisa.
Msingi wa kutotaka ujamaa na Israel ulikuwa zaidi ya matakwa ya kidini na fikra za kawaida. Ulilenga kuonesha kutokukubaliana na siasa za Mashariki ya Kati.
Israel kwa Palestina tofauti yake ni ndogo na hali ilivyokuwa Afrika Kusini ya makaburu na jinsi ambavyo Wazungu waliwanyanyasa kibaguzi Waafrika wa nchi hiyo.
Ndiyo sababu haikuwa na mantiki kuwanyooshea kidole makaburu wa Afrika Kusini kisha kuwachekea Waisrael kwa Palestina. Na ikawa sababu kwa hati ya kusafiria ya Tanzania miaka ya nyuma kuweka zuio la kwenda Afrika Kusini na Israel.
Ushauri kwa Dk. Magufuli ni kuizingatia misingi iliyowekwa na waasisi wetu. Walipokataa jambo, hawakukurupuka, walikuwa na sababu na waliweza kuzisimamia.
Ni lazima atambue kwa ndani kabisa ushiriki wa Tanzania katika siasa za Kimataifa. Ayaelewe na kuyazingatia mataifa ambayo yana urafiki wa asili na nchi yetu. Vilevile awajue na awe macho na maadui wa chinichini.
Nchi zote huwa na sera zoa za kimataifa. Unaweza kushangaa ni kwa nini Ronald Reagan aligombana na Muammar Gaddafi miaka ya 1980, ugomvi huo ukaendelea kuwepo mpaka utawala wa Barack Obama na kushiriki kumuua.
Mathalan, haiwezekani Rais wa 45 wa Marekani, aibuke kivyakevyake bila kupitia bunge (Congress) kisha aamue kuitangaza Iran kama taifa rafiki. Haitaweza kutokea hali hiyo.
Rais wa Rwanda, Paul Kagame amekuwa akitajwa katika kashfa ya kupandikiza utawala wa Hima (Hima Empire), na hiyo ikawa sababu ya kuanzisha vita baridi na Tanzania.
Chokochoko za waasi wa M23 kusumbua DRC na kutishia Tanzania, ni mambo ambayo yalionekana moja kwa moja kuwa na mkono wa Kagame, kiasi cha kuwepo tishio la vita.
Haiwezekani ghafla tu baada ya Kikwete, Kagame awe rafiki pendwa wa Tanzania chini ya Dk. Magufuli.
Tunakumbuka mipango ya kuvuruga Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Kagame kufanya ushikiano na Yower Museveni wa Uganda na Uhuru Kenyatta wa Kenya, kisha kumtenga JK kwa Tanzania na Pierre Nkurunziza wa Burundi.
Tulishasikia magari ya Tanzania kuzuiwa Rwanda au kutozwa ushuru na kodi kubwa. Kenya ikaiga lakini walinywea haraka baada ya Tanzania kupunguza safari za ndege za Shirika la Anga la Kenya (Kenya Airways).
Hata machafuko ya Burundi Kagame anatajwa katika jaribio lake la kusimika utawala wa Hima, kwamba hata Tanzania alijitahidi sana kuwekeza fedha kwa Edward Ngoyai Lowassa. Kagame hawezi kuwa rafiki wa Tanzania ghafla!
Mambo ya ushirikiano wa kimataifa, ningemshauri Dk. Magufuli awe analifanya kuwa jambo nyeti, na ikiwezekana kulihusisha bunge.
Dk. Kikwete alipoona mambo ni mvurugiko kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, alikwenda bungeni kuelezea hali halisi. Huo ndiyo utaratibu mzuri, siyo serikali na mamlaka yake tu, bunge ni lazima kushirikishwa.
Mathalan, suala la Israel ingekuwa vizuri lingejadiliwa na bunge, tuone misimamo ya wabunge ipoje, kwa kutazama maazimio ya mwanzoni na hali ya kisiasa iliyopo sasa.
Ushauri wangu pia kwa bunge, ni kutambua nafasi yake. Siyo kugeuka mashabiki au wagonga meza wa kusherehekea uamuzi wa serikali. Lazima kujadili na kupitisha au kukataa mambo nyeti. Uamuzi wa Magufuli kuhusu Israel umesaliti msingi wa waasisi wetu.

No comments:

Post a Comment

Featured post

MWANAMKE YAFUATE HAYA; NI MUHIMU KWA MAHUSIANO YAKO

1. Degree yako ya fist class uliyoipata chuo kikuu haiwezi kukufanya uwe mke first class katika ndoa yako bali ni heshima yako na uthubu...