Monday, 7 August 2017

NAMNA MWANAMKE ANAVYOWEZA KUTUMIA NAFASI ZAKE KUBADILISHA MAISHA YA NDOA YAKE



Mithali 14: 1 “Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe”.

Padre mmoja rafiki yangu aliniambia asilimia hamsini mpaka sabini ya changamoto au matatizo anayoshughulika nayo mara kwa mara ni ya wanandoa. Kwa Binafsi lugha nyepesi asilimia 50 – 70 ni matatizo yatokanayo au yanayohusiana na ndoa. pia kwa upande wangu kupitia kuperuzi kwenye mitandano, email za wasomaji ninazopata na pia baadhi ya tafakari na wanandoa kadhaa kuhusu eneo hili nimegundua kwa hakika ndoa nyingi za wana wa Mungu zina shida na wao hawajajua kwamba vita hii inatoka kwa Shetani, maana anajua ndoa zikitengamaa ni faida kwa ufalme wa Mungu na ni uharibifu kwenye ufalme wake wa giza. Naam anapigana usiku na mchana ili kuhakikisha ndoa hazitengamai kwa kuleta fujo za kila aina.

Kila siku katika ndoa kuna changamoto zinazaliwa mpaka imefika mahala baadhi ya wanandoa wanawaza kwa nini walikubali kuoa au kuolewa. Kwa hakika laiti Biblia ingetoa mwanya kwa wanandoa kuachana basi kuna baadhi ya wanandoa wangehakikisha wanaitumia hiyo nafasi vizuri kwa kuwa ndoa zimegeuka ndoano. Matarajio ambayo kila mmoja alikuwa nayo kwenye ndoa anaona hayatimii. Kinachosumbua watu wengi ni kwamba kabla hawajaonana hawakujua nini kinakuja kupitia ndoa, hawakuweza kuona uhalisia wa maisha ya ndoa utakuwaje? Bali kila mmoja alikuwa na mtazamo/fikra na matarajio yake binafsi juu ya ndoa yake.

Naam zipo sababu nyingi sana zinazopelekea matatizo au changamoto kwa wanandoa. Katika kitabu hiki nitaandika zaidi zile zinazotokana na upinzani kutoka kwa Shetani ili kuathiri kusudi la Mungu. Lengo la ujumbe huu ni kukufundisha wewe mama (Mwanandoa) namna ya kuzitumia ‘nafasi’ ambazo Mungu amekupa Kibiblia ili kuiponya ndoa yako au kubadilisha hali ya sasa ya ndoa yako endapo unaona si ile ambayo Mungu amekusudia.

Kwa nini Mwanamke?

Pengine utaniuliza kwa nini mwanamke ndiye awajibike katika kuponya au kubadilisha maisha ya ndoa yake? Binafsi katika kuisoma Biblia na stadi mbalimbali nimegundua kwamba kwa kuzingatia nafasi ambazo mwanamke amepewa kibiblia ni ishara ya kwamba kwa habari ya ndoa, Mwanamke ana nafasi kubwa ya kuijenga au kuibomoa ndoa yake na hivyo nyumba yake kwa ujumla. Mara kwa mara Mungu ananifundisha masuala ya wanawake, suala la wanawake kuwa kwenye ‘nafasi zao’ husisitizwa sana.

Kwa nini nafasi?

Sijui kama unafahamu maana ya nafasi ambayo Mungu anampa mtu katika ulimwengu wa roho. Hizi ni nafasi ambazo Mungu amekupa wewe mawanamke katika ulimwengu wa roho ili uzitumie kufanikisha kusudi lake kupitia ndoa yako. Nafasi (position) ni eneo ambalo mtu anapaswa kuwepo kwa kuhusianisha na vitu au watu wengine, naam ni wadhifa ambao mtu anakuwa nao kwa kuhusianisha na mtu au watu wengine.

Kwa hiyo hizi ni nafasi ambazo Mungu amempa mwanamke zikihusiana na mwanaume katika kilitumika kusudi la Mungu hapa duniani. Mwanamke anapokuwa amesimama katika nafasi zake ndipo anapoweza kuruhusu mawazo ya Mungu kupitia ndoa yake kutimia naam ndivyo anavyoweza kuzuia mawazo ya Iblisi kupitia ndoa yake yasitimie. Naam nafasi ya mwanamke katika ndoa ndiyo inayoamua uzima au mauti ya ndoa yake, nafasi ndiyo inayopelekea kufanikiwa au kufeli kwa ndoa yake, nafasi ya mwanamke katika ndoa ndio inayoamua nini kingie au kitoke kwenye ndoa.

Katika kusoma kwangu Biblia na uzoefu katika kusoma maeneo mbalimbali, nimegundua kwamba Mungu amempa nafasi zifuatazo mwanamke;

o Mwanamke kama ‘msaidizi’ wa mumewe

o Mwanamke kama ‘mlinzi’ wa mwanaume

o Mwanamke kama ‘mjenzi’ wa nyumba yake

o Mwanamke kama ‘mshauri’ wa mumewe

o Mwanamke kama ‘mleta kibali’ kwa mumewe



Mwanamke kama Msaidizi

Mwanzo 2:18 ‘BWANA Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye’. Ukisoma mstari huu katika toleo la GNB Biblia inasema ‘Then the LORD God said, “It is not good for the man to live alone. I will make a suitable companion to help him.” Biblia inatueleza kwamba Adam ndiye aliyetangulia kwanza kudhihirishwa kabla ya Mwanamke. Kabla ya Hawa kuletwa, Mungu alimpa Adam majukumu mengi ambayo alipaswa kuyatekeleza.

Katika kutekeleza majukumu yake Adam aliona kwamba amepungukiwa mwenza wa kufafanana naye na ndani yake akatamani angepata mtu wa kuwa naye karibu kwa kila afanyalo. Ukweli huu tunaupata tukisoma Mwanzo 2:20 kwamba ‘Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. Naam kutokana na upweke wa Adam ndipo Mungu akamfanya Hawa mkewe kama msaidizi. Kitendo cha Mungu kumfanya mwanamke kama msaidizi ni ishara kwamba Mungu alijua kuwa Adam hawezi kuwa na ufanisi mzuri katika kutekeleza majukumu (Kusudi) aliyopewa bila mwenza wa kufanana naye.

Maandiko yanasema kwamba ‘Maana mwanaume hakutoka katika mwanamke, bali mwanamke katika mwanaume. Wala mwanaume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanaume’ (1Wakorinto 11:8-9). Ile kwamba mwanamke aliumbwa kutoka kwa mwanaume na kwa ajili ya mwanaume ni kuonyesha kwamba wajibu au nafasi mojawapo ya mwanamke ni kuwa msaidizi wa mumewe. Hata hivyo neno msaidizi halipaswi kutafsiriwa vibaya na kuonyesha kwamba mwanamke hana thamani.

Mwanamke ni msaidizi wa mume katika kulitumikia kusudi la Mungu isipokuwa kinacho watofautisha ni utendaji wao tu. Mume hapaswi kumdharau mkewe wala mke kumdharau mumewe kwa kuwa mume si mume bila mke na mke si mke bila mume, wao ni mwili mmoja, kusudi lao ni moja na BWANA wao ni mmoja. Maandiko yafuatayo yanaonyesha baadhi ya mambo ambayo mwanamke anapokuwa katika nafasi ya Msaidizi anapaswa kuyafanya;

Tito 2:4 inasema ‘Ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao, na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe’.

1 Timotheo 5: 14 ‘Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, wawe na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu’. Ukisoma pia katika 1 Wakorinto 7:4a kwa habari ya tendo la ndoa Biblia inasema ‘Mke hana amri juu ya mwili wake…’ na mstari wa 5a unasema’ Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda…, Naam hii ina maana kama mke ataweka amri kwa habari ya tendo la ndoa kwa mumewe ajue kabisa ameshindwa kumsaidia mumewe na kuna hatari ya kuanguka kwenye zinaa. Naam Mungu anataka akina mama walioko kwenye ndoa wajifunze kuwasaida waume zao wasiingie kwenye zinaa.

Naam hata sasa ni muhimu sana wewe mama ukajua Mungu amewaunganisha ili kufanya nini hapa duniani kwa ajili ya ufalme wake. Changamoto kubwa iliyipo leo ni kwamba wanandoa wengi wameingia kwenye ndoa kwa sababu ni desturi ya wanadamu kuoa na kuolewa. Wengi wameshindwa kuunganisha suala la kuoa au kuolewa na kumtumikia Mungu kupitia ndoa yao. Mungu anapokuunganisha na mumeo maana yake anakupeleka kwenye wajibu wa kuwa msaidizi kwa mumeo. Naam hakikisha kwamba unafanyika msaada kwa mumeo kwa namna ambayo kile ambacho mnajua kwamba Mungu amewapa kukifanya hapa duniani kinafanikiwa. Zaidi unaweza soma Mithali 31:10-31 ili kuongeza ufahamu zaidi kuhusu nafasi ya mwanamke kama Msaidizi.

Mwanamke kama Mshauri

Katika hali ya kawaida watu wengi hutafsiri mshauri kuwa msiaidizi. Kwa kuzingatia dhana ya nafasi katika ulimwengu wa roho imenilazimu kutenganisha ili kukuonyesha umuhimu wa nafasi ya mwanamke kama Mshauri. Biblia katika Mithali 31:26 inasema ‘Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake’.

Naam andiko hili linatupa kujua kwamba Mke ndiye mshauri mkuu wa mumewe. Siri moja ya mwanamke kuwa mshauri mzuri ni kuwa na ufahamu wa kutosha wa neno la Mungu. Hivyo kama Mke hana hekima itokanayo na neno la Mungu kwa wingi ndani yake, hawezi kuwa mshauri mzuri. Ushauri unategemea nguvu za ufahamu alizonazo Mwanamke, kadri anavyokuwa na ufahamu wa kutosha wa neno ndivyo anavyokuwa kwenye nafasi ya kutoa ushauri bora kwa mumewe.



Biblia katika kitabu cha Mithali 8: 14-16 inasema ‘Shauri ni langu, na maarifa yaliyo sahihi; Mimi ni ufahamu na mimi nina nguvu. Kwa msada wangu wafalme humiliki, Na wakuu wanahukumu haki. Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia’. Fahamu kwamba hekima ndani yako mama itakupa maarifa na ufahamu wa kumshauri mumeo ili kufanya maamuzi sahihi katika kila atendalo. Hekima ni sawasawa na shauri/maarifa/ufahamu/nguvu. Ukiona kiongozi yoyote anatawala/anaongoza watu vizuri ujue washauri wake wanamshauri vizuri au ujue ana wahsauri wazuri. Vivyo hivyo mwanaume anafanya kazi zake vema na kufanikiwa katika yale atendayo ujue nyuma yake kuna mwanamke mwenye nguvu za ufahamu anayemshauri vema.

Naam chanagmoto au matatizo mengi yaliyopo kwenye ndoa leo ni matokeo ya akina mama kukosa hekima itokanayo na neno la Mungu ya kuwashauri waume zao. Wengi wanategemea akili zao, au ushauri wa rafiki zao nk. katika kuangalia ndoa zao na mambo yao yaendaje. Kutegemea ushauri wa watu wengine bila wewe mwenyewe mama kutafuta hekima itokanayo na Mungu kwanza inaweza kukufikisha kupata ushauri wa kipepo kama ilivyomtokea Hawa pale Bustanini. Kumbuka Mshauri ni mtoa taarifa, mtoa pendekezo juu ya nini mume wake aweza fanya au kutofanya.

Mwanamke kama mleta kibali.

Hii ni nafasi ya ajabu sana ambayo Mungu amempa mwanamke. Mwanamke anapokuwa kwenye hii nafasi mambo matatu yanafanyika; 1) Mume anaingia kwenye ngazi ya kushirikishwa siri/mambo/majukumu mengi kutoka kwa BWANA. 2) Kukubalika kwa mume wake katika jamiii/kazi/kanisa nk kunaongezeka 3) Na mwisho maombi ya mume wake yanasikilizwa. Mambo haya yanathibitishwa na Biblia katika Mithali 18:22 inayosema ‘Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa BWANA’, pia Mithali 31: 23 inayosema ‘Mume wake hujulikana malangoni; Aketipo pamoja na wazee wa nchi.

Zaidi kwa habari ya maombi ya mume kusikilizwa au kutokusikilizwa Biblia katika 1 Petro 3:7 inasema ‘Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe’. Naam hii ni ishara kwamba mke anaweza kusababisha maombi ya mumewe yakasikilizwa au yasisikilzwe. Unaweza ukafikiri hili andiko linawahusu akina baba pekee, lakini ukilitafakari kwa upana utagundua kwamba linawahusu akina mama pia ili wajue kwamba kuwa mke ni nafasi ambayo inaweza kuzuia maombi/baraka/majibu au kukwamisha mafanikio ya waume zao kama hawatukuwa makini katika kuwasaidia waume zao kuishi nao kwa akili.

Si wengi wanaojua kwamba kuna maombi mengi ya familia/waume zao hayajibiwi kwa sababu maombi ya mume ambaye ndiye kichwa hayasikilizwi na Mungu. Na chanzo cha kutokusikilizwa ni kuharibika kwa uhusiano kati ya mume na ‘mleta kibali’ wake yaani mke. Hivyo wewe mama mwenye ufahamu huu jifunze kwenda mbele za Mungu na kuomba toba kwa ajili ya mumeo mara kwa mara. Kwa sababu kuna vitu au maamuzi anayoweza kufanya nay eye akaona yuko sahihi lakini kumbe ni uamuzi ambao unajenga ukuta kati ya maombi yake na Mungu wako.





Hakikisha unasimama vema kwenye hii nafasi ili Mungu alete uponyaji kwa mume wako na maombi yake yaweze kusikilizwa. Naam simama kwenye nafasi yako ili kumjengea mazingira mazuri mumeo ya kuishi na wewe, ndivyo na maombi yake yatakavyosikilizwa, ndivyo atakavyopata kibali mbele za BWANA, naam atakuwa mume bora katika jamii na kufanikiwa katika kila atendalo.

Endapo mwanamke atakaa vizuri kwenye nafasi hizi haijalishi mume wake ni mgumu kiasi gani, mama akizungumza kwa maana ya maonyo au ushauri lazima mwanaume asikilize au kufuata kile ambacho msaidizi, mlinzi, mleta kibali wake nk anamweleza, na kama akikataa uharibifu ni haki yake. Mungu ameweka sauti ndani ya mwanamke ambayo inaweza kuleta uponyaji kwa mumewe endapo mwanamke atakaa vizuri kwenye hizi nafasi.


Mwanamke kama Mlinzi

Labda nianze kwa kuuliza, je una fahamu kwamba wajibu wa kumlinda mumeo ni wako? Naam Mungu amejiwekea utaratibu mpya kwamba Mwanamke amlinde mwanaume. Je ni ulinzi wa namna gani? Ni ulinzi wa kiroho ndio ambao mwanaume anahitaji kutoka kwa mkewe. Mke anatakiwa kuwa makini ‘sensitive’ katika ulimwengu wa roho kuangalia ni mashambulizi gani Shetani amekusudia kuyaleta kwa mume/ndoa yake. Naam akishajua aweke ulinzi ili mawazo ya Shetani yasitimie kwenye ndoa yake.

Kuwa Mke wa fulani, ni nafasi ya ulinzi katika ulimwengu wa roho ambayo Mungu anaitoa. Kwa hiyo fahamu kwamba unapoingia kwenye ndoa, Mungu anakupa wajibu wa kumlinda mumeo. Biblia katika Yeremia 31:22 inasema ‘Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana BWANA ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanaume. Nafasi ya ulinzi ni nafasi ya pekee sana ambayo Mwanamke amepewa na endapo ataitumia vizuri itamsaidia kweli kweli kuiponya ndoa yake. Hii ni kwa sababu mlinzi ndiye anayeona mambo yanayotaka kuja kwenye ndoa yake akali kwenye ulimwengu wa roho, kabla hayajadhihirika kwenye ulimwengu wa mwili.



Ukisoma Mstari huu wa Yeremia 31:22 katika toleo la kiingereza la ESV unasema ‘How long will you waver, O faithless daughter? For the LORD has created a new thing on the earth: a woman encircles a man’ na pia katika toleo la KJV imeandikwa ‘How long wilt thou go about, O thou backsliding daughter? for the LORD hath created a new thing in the earth, A woman shall compass a man’. Maneno ‘Mwanamke atamlinda mumewe’ kwenye ESV imeandikwa ‘a woman encircles a man’ na kwenye KJV imeandikwa ‘A woman shall compass a man’. Maneno haya yana maana ya zingira, zunguka au fanya duara.

Hapa Biblia inajaribu kutueleza jambo la mwanamke ambaye yamkini kutokana na changamoto za ndoa yake/mume wake alijikuta amekuwa mtu wa kuasi/kufanya mabaya. Sasa ili kumsaidia ndipo BWANA akamtuma Yeremia kumweleza ‘acha kutanga tanga, Mungu ameumba jambo jipya nalo ni ‘wewe mwanamke, umepewa wajibu wa kumlinda/kumzingira mwanaume/mumeo’. Naam ulinzi huu ni kwa jinsi ya rohoni. Mwanamke anaweza kumwekea/kumfanyia mume wake ulinzi dhidi ya makahaba, malaya, wenye hila, wala rushwa au chochote ambacho ni chanzo cha uharibifu wa ndoa nk.

Katika nafasi hii ya ulinzi Mke una wajibu wa kujua kwa nini Mungu amekuunganisha na mume uliye naye sasa. Naam lipo kusudi la ufalme wake, hivyo ni jukumu lako kuhakikisha linatimia katika siku zenu za kuwepo hapa duniani kama wanandoa. Naam msaidie Mume wako kama Mlinzi kwa namna ambayo kusudi la Mungu halitakwama kwenye maisha yenu. Fahamu kazi ya Mlinzi ni kumsaidia Bwana wake kufanikisha majukumu yake. Endapo Mlinzi hatakuwa makini kwenye nafasi yake basi majukumu ya Bwana wake hayatafanikiwa, si kwa sababu ametaka bali ni kwa sababu Mlinzi/Walinzi wake hawakumpa usaidizi wa kutosha kiulinzi.

Ni vizuri ukafahamu kwamba ili Shetani ammalize mumeo, njia kuu kwake ni kupitia kwa mkewe. Angalia leo ndoa ngapi zimeharibika na ukifuatilia chanzo utagundua Mke amechangia kwa sehemu kubwa. Hebu taunaglie mifano kadhaa ndani ya Biblia;

Ndoa ya Anania na Safira (Matendo ya Mitume 5:1-11).

Ule msitari wa 1-2 maandiko yanasema ‘Lakini Mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali, akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume’. Ukisoma fungu zima hapo juu utagundua kwamba kutokana na wizi wao wote wawili, walikufa siku moja. Jambo ninalotaka tulione hapa ni ile kusema ‘mkewe naye akijua haya’. Maneno haya yameandikwa ili kuonyesha namna ambavyo Safira hakutumia nafasi yake kuiponya ndoa yake. Kutokana na kutokumshauri mumewe vizuri na kumlinda dhidi ya hatari iliyokuwa mbele yao, wote wawili walikufa. Nani ajuae kwamba pengine Safira angemwonya mumewe, mumewe angemsikiliza. Naam kwa kuwa alinyamaza, na Mungu alinyamaza, mauti ikawajia.

Ndoa Ahabu na Yezebeli (1Wafalme 21:1-23)

Ukisoma andiko hili utaona namna Yezebeli mke wa Ahabu alivyotumia vibaya nafasi zake, kwa kumuua Nabothi ili amrithishe mumewe shamba la Nabothi. Biblia katika mstari wa 9 -10 inasema Yezebeli Akaandika katika zile nyaraka, akasema, pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki na kumshuhudia, kunena, umemtukana Mungu na mfalme, kisha mchukueni nje mkampige kwa mawe, ili afe’. Watu wa mji walifanya kama Yezebeli alivyoagiza. Naam Yezebeli hakujua huo ndio ulikuwa mwisho wa utawala wao kwa kosa lile, kwani mahali pale ambapo mbwa waliramba damu ya Nabothi ndipo na damu ya Ahabu ilipomwagika wakairamba pia. Naam angekuwa na ufahamu huu, angetumia nafasi zake vizuri kuponya ndoa yake na utawala wao juu ya nchi.

Ndoa ya Abramu na Sarai (Mwanzo 16:1- 6) nk.

Kutokana na Sarai kutokupata mtoto kwa miaka mingi alimshauri Abramu mumewe atembee na mjakazi wake aliyeitwa Hajiri pengine angepata mtoto. Maandiko yanasema Abramu akaingia kwa Hajiri naye akashika mimba. Kitendo cha Hajiri kushika mimba kikamfanya Sarai aonekane duni/asiyefaa mbele za Hajiri. Ndipo Sarai akamwambia mumewe kusema ‘ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. BWANA na ahukumu kati ya mimi na wewe’. Maandiko hayatuelezi endapo Abramu aliwahi kumwambia mkewe kwamba unipe mjakazi wako nimwingie ili kukuzalia mtoto. Lilikuwa ni wazo la Sarai, naam akalitekeleza, bila kujua matokezo ya mawazo yake ni nini. Ukiendelea kusoma Biblia utagundua kwamba jambo hili liliwakosanisha Sarai na Hajiri, si hivyo tu lakini hata ndoa yake iliathirika. Laiti angedumu kwenye ahadi ya Mungu, fedheha aliyoipata isingemtokea.

Ee Mwanamke, Je umeona jinsi wanandoa hawa yaani Safira, Yezebeli na Sarai walivyotumia vibaya nafasi zao? Ni Wake wangapi leo wanafanya mambo yanayofanana na haya kwa kujua au kutokujua? Ndoa ngapi leo zipo kwenye matatizo kwa kuwa Wake wanawadharau waume zao? Ndoa ngapi leo zimeharibika kwa sababu Wake hawawashauri vema waume zao juu ya Zaka na Sadaka? Ndoa ngapi leo zimeharibika kwa kuwa Wake hawataki kuwapa waume zao haki ya tendo la ndoa? Ndoa ngapi leo zinaharibika kwa sababu Wake wanawaunga mkono waume zao kufanya yaliyo maovu? Naam imefika mahala Wake wanakubali kufanya zinaa kinyume na maumbile na waume zao? Naam ndoa ngapi leo zimeharibika kwa kuwa wanawake hawapo kwenye nafasi zao kama Wasaidizi, Washauri, Waleta kibali na Walinzi, na hivyo Shetani anatumia uzembe wao kuharibu ndoa zao? Naam baadhi ya akina mama wanafanya mambo mabaya kwa lengo la kuwapendeza waume zao, wasijue kadri wanavyotoka nje ya nafasi zao kiroho, ndivyo adui anavyopanda uharibifu kwenye ndoa zao ili kukwamisha kusudi la Mungu kupitia ndoa zao.

Mambo ya muhimu kwa mwanamke kujua kuhusiana na nafsi ya kuwa mlinzi ni 

a) Mke amepewa/amefanywa kuwa ‘Mlinzi’ wa ‘Mume’ katika ulimwengu wa roho hapa duniani.

b) Ni wajibu wa Mke kama ‘Mlinzi’ kusimama kwenye nafasi yake ili kuhakikisha kusudi la Mungu linafanikiwa kupitia ndoa yake 

c) Ili Mungu ampe Mke taarifa kuhusu mumewe na nyumba yake, Mke sharti awe kwenye nafasi yake maana Mungu hua anatoa taarifa kwa walinzi tegemeana na ‘nafasi zao’ 

d)Mke anapasawa kuitumia ‘taarifa’ anayopewa na Mungu kama ‘fursa’ ya uponyaji wa ndoa yake.

Wake wengi leo wamebaki kuwalaumu waume zao kutokana na mambo wanayoyafanya ili hali wao hawafanyi pia wajibu wao. Je mara ngapi kwa siku unamuombea mumeo kwa kumaanisha? Ni ulinzi kiasi gani umemuwekea mumeo? Je unafafamu kwamba suala la usalama wa mume wako, Mungu ameliweka kwako? Naam usipofanya na Yesu hafanyi? Ukinyamaza na yeye ananyamaza? Unajua kwa nini? Ni kwa sababu Mungu hawezi kuweka ulinzi juu ya mji, kama Mlinzi wa mji hajasema ‘BWANA linda mji huu’ (Isaya 62:6-7). Naam Jenga nidhamu ya kuomba kila siku kwa ajili ya mumeo ili Mungu aachilie ulinzi wake juu ya mumeo kwa kuwa wewe, kama Mlinzi uliyeko kwenye nafasi, umeshauri na umeelekeza kufanya hivyo. Naam ni wajibu wako pia kutumia damu ya Yesu kumwekea mumeo ulinzi kwenye kila eneo la misha yake na hivyo kuiponya ndoa yako (Asomaye na afahamu).

Mwanamke kama Mjenzi

Biblia katika kitabu cha Mithali 14:1 inasema ‘Kila mwanamke aliye na hekima huijenga nyumba yake: Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe’. Tafsiri ya neno nyumba ni familia, naam na familia inajumuisha baba, mama na watoto endapo mmejaliwa. Hata hivyo katika hali ya kawaida watoto watalelewa katika msingi mzuri endapo ndoa husika imetengamaa. Ifahamike kwamba hili andiko si la wanandoa peke yao, bali hata wanawake wasio wanandoa wenye familia kama wajane, walezi nk linawahusu. Kwa kuwa hapa tunazungumzia habari za wanandoa nitalifafanua zaidi kutoka kwenye kona hiyo. Pia neno nyumba limetumika ili kutupatia urahisi wa kuelewa namna nyumba za kawaida zinavyojengwa ili tueguze dhana hiyo kiroho pia. Kwa lugha rahisi ndoa yako ni nyumba, hivyo ubora, uzuri na mvuto wa ndoa yako unategemea namna unavyoijenga daima kwa hekima.

Ni vizuri ukafahamu kwamba suala la ujenzi/maboresho ya ndoa yako ni jukumu la kila siku ya kuishi kwa ndoa yenu mpaka kifo kiwatenganishe. Kila mmoja katika ndoa ni lazima ahakikishe anasimama kwenye nafasi yake na kufanya yale yampasayo ili kuifanya ndoa yake kuwa bora zaidi. Endapo hakutakuwa na jitihada za wanandoa katika kuimarisha ndoa yao, Shetani atatumia fursa hiyo kuivuruga ndoa husika. Kujenga kunakozungumziwa hapa ni kule kuhakikisha ndani ya ndoa kuna mahusiano na mawasiliano mazuri baina yenu ambayo yatafanikisha kutekelezwa kwa kusudi la Mungu.





Ukweli wa ajabu na wa pekee

Ni ajabu sana kuona kwamba jukumu la ujenzi wa ndoa/nyumba amepewa mwanamke. Hii haina maana mwanaume hahusiki, hapana, bali ki-nafasi jukumu la ujenzi wa nyumba/ndoa ni la kwako mama. Kumbuka nilikueleza kwamba nafasi hizi tano za Mwanamke katika ndoa zinafanya kazi kwa pamoja na kwa kutegemeana. Katika nafasi hii ya ujenzi unapaswa kuhakikisha unajenga ndoa yako ili kuzuia kila ufa/fursa ambayo Shetani anaweza kutumia kuvuruga ndoa yako. Kumbuka katika hali ya kawaida kujenga ni kuimarisha/kuweka mazingira bora juu ya kile unachokithamini ili kuzuia madhara yanayoweza kutokea. Naam nafasi hii inalenga kukusaidia uwe makini sana na kila kinachoweza kubomoa ndoa yake.



Suala la ujenzi wa ndoa ni endelevu kwa sababu siku zote adui anatafuta kubomoa ndoa yako. Ni lazima uwe makini kujua wapi ni mahali palipobomoka ambapo Shetani anapatumia sasa kuharibu ndoa yako au anaweza kutumia baadaye kuharibu ndoa yako, naam ukishajua kwa kutumia hekima, jenga ukuta imara ambao adui hawezi penya. Kama ndoa yako ina nyufa basi ni rahisi adui kupita kwenye hizo nyufa. Kumbuka hata kama umemaliza kujenga kila kitu kwenye nyumba yako, bado kuna matengenezo ya mara kwa mara yanahitajika ili kuifanya nyumba yako kudumu katika hadhi inayostahili. 


MAENEO YA MSINGI KATIKA KUJENGA NDOA YAKO

Utiifu kwa mumeo

Maandiko yanasisitiza sana wanawake kuwatii waume zao (Waefeso 5:22-24, 1 Petro 3:1). Mitume walindika maandiko haya ili kuwaonya wanawake kutokana na mienendo yao mbele za waume zao kitabia na hasa katika suala zima la utiifu. Bahati mbaya baadhi ya akina mama sio watiifu kwa waume zao na tena wengine wana dharau kubwa sana. Naam fahamu kwamba Mke si Mke bila ..................................

Kuendelea kupata mambo haya na elimu zaidi kuhusu ndoa nipigie kupitia 0767141643 au email yangu mmassyfm@yahoo.com.

Karibu tuendelee kujifunza

No comments:

Post a Comment

Featured post

MWANAMKE YAFUATE HAYA; NI MUHIMU KWA MAHUSIANO YAKO

1. Degree yako ya fist class uliyoipata chuo kikuu haiwezi kukufanya uwe mke first class katika ndoa yako bali ni heshima yako na uthubu...