Katika Injili ya Luka 16:18 “Kila amwachaye mkewe na kumuoa mke mwingine azini naye amwoaye yeye aliyeachwa na mumewe azini.”
Nimesukumwa kulizungumzia suala hili zito: Suala la kuachana
watu wawili waliokwisha kuoana, waliokwisha kukubaliana kuwa MKE na MUME.
Maandiko yamesema hapo juu kuwa kila amwachaye na kuoa mwingine “AZINI”, na yule amwoaye yule aliyeachwa AZINI.
Kwa hiyo katika mafundisho ya Kikristo yanayojengwa katika misingi ya
Biblia,kuachana ni jambo lisilo ruhusiwa kimaandiko.Msingi wa haya unatokana na
ukweli kwamba Mwanaume na Mwanamke waliooana wanahitajiana katika suala zima la
kimaumbile.Hivyo kuachana kunatoa mwanya kwa kila mmoja kutafuta hitaji hilo la
kimwili sehemu tofauti na pale ambapo paliahalalishwa.
Ukisoma Waefeso 5:33 “Lakini kila mtu ampende mke wake kama
nafsi yake mwenyewe, na mke asikose kumstahi mumewe”
Mpendwa, hebu tuendelee kujifunza kutoka kwenye Neno la Mungu.
Wajibu wa MUME ni kumpenda mke wake kama nafsi yake(kama unavyojipenda). Suala
hili ni gumu; ni agizo gumu, lakini aliyetuagiza anajua kuwa wanaume wataweza
kumpenda mke kama mtu apendavyo nafsi yake. Mtu anapojikwaa mguu, kwa kuwa
anaupenda mguu wake, haupigi, wala haukati, anaupuliza, anaushughulikia kama
umeumia, hawezi kuuliza kuwa ‘ulikuwa unatembeaje mpaka ukajikwaa?’. Na MKE
ameambiwa asikose KUMSTAHI mumewe. KUMSTAHI ni KUMHESHIMU MUMEWE.
Kumheshimu kwa njia gani?
Jibu linapatikana katika kitabu cha Waefeso 5:22 “Enyi
wake watiini waume zenu, kama kumtii Bwana wetu, kwa maana mume ni kichwa cha
mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha kanisa, naye ni mwokozi wa mwili. Lakini
kama vile kanisa limtiivyo Kristo, viyo hivyuo nao wawatii waume zao katika
kila jambo”
Twende tukijifunza, ili ndoa zipone maana nyingi zimeoza, hazifai.
Wamama wameambiwa wawatii waume kama kumtii Kristo,Tukumbuke kuwa Mwanaume ni
kichwa. Sasa kama mume ni kichwa, ndiye anatakiwa kuongoza nyumba, kwa kuwa
kichwani kuna- MACHO, MASIKIO, UBONGO, MDOMO, n.k
Naandika mambo ya kimaandiko, wamama wengi wamebomoa nyumba zao
kwa mikono yao, pale walipojaribu kuongoza, wakidhani wanaweza. Kumbuka neno
linasema kuwa Adamu aliishi bila Hawa lakini Hawa hakuwahi kuishi bila
Adamu. Hawa alipoishi bila Adamu kwa dakika chache tu aliondoka
akakutana na nyoka, wakati Adam hayupo pamoja naye, akajitahidi kuzungumza na
nyoka akijibu maswali aliyokuwa anaulizwa, lakini alishindwa.
Biblia inasema katika 1Timotheo 2:13-14 “Kwa maana Adamu
ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye. Wala Adamu hakudangaywa, ila mwanamke
alidanganywa kabisa, akaingia katika hali ya kukosa”
Biblia inaeleza wazi wazi kuwa Adam hakudanganywa. Aliyedanganywa
ni Hawa. Sasa tuendelee kujiuliza: kama Adam hakudanganywa, ilikuwaje Ale
tunda? Je, Alilazimishwa?;Na kwa nini alikula?
Nilipokuwa natafakari mambo haya niliyaona kwa ndani zaidi.
Utakumbuka wakati Bwana alipokuja ili akutane nao Bustanini, hakuwakuta,
akamwita Adam na kumuuliza alikokuwa! Adamu akasema “nimejificha, kwa
kuwa niko uchi”; akamuuliza “nani amekwambia kuwa uko uchi?” [au umekula tunda
nililokukataza?] Adamu akasema “Mwanamke uliyenipa ndiye amenipa tunda nikala”.
Sasa ona hapa, Je, Hawa alimlazimisha? Kwa nini
alikula? Watu wengi wanasema kuwa Adam aliposema kuwa ni huyo mwanamke
uliyenipa, alikuwa anamlaumu Mungu kwa kumpatia
mwanamke. Hapana! Hebu nikufundishe kitu hapo kupitia kitabu hiki :
Biblia inasema “Apataye mke apata kitu chema, tena hujipatia kibali kwa Bwana”
Sasa Adam alipojibu kuwa “ni huyo mwanamke uliyenipa” alikuwa
akisema hivi: “Huyu mwanamke uliyenipa, najua hukunipa kitu kibaya, ulinipa
kitu chema kabisa Ee Mungu wangu, na mimi kama mimi hajanikosea, amekukosea
wewe. Na kwa kuwa wewe Mungu wangu ulinipa kitu chema basi sitakiacha,
nitaongozana nacho kokote kitakakokwenda, sitakiacha. Wewe Mungu una uwezo,
kwanza unajua kuwa ni chombo dhaifu, wewe ungeweza kukizuia kabisa kisile tunda
lakini ukakiacha kikala, basi nakufa nacho!”.
Alipomaliza kusema hayo akalipokea tunda kwa hiari yake,
akala na akajua sasa hawawezi kumuona Mungu wakiwa na hali hiyo;
wakakubaliana waondoke shambani.
Sababu nyingine iliyofanya ale ni kuwa alijua kuwa yeye Adam
aliishi bila Hawa na wala hakuomba Mungu ampe mke, ni Mungu tu alisema
“si vema sasa uwe peke yako nitakufanyia msaidizi”, na akamfanyia wa
kufanana naye, yaani alimfanyia mwili wake, sasa mwili wako utaukataaje uutupe?
Akajua kuwa UBAVU wenyewe hauwezi kuishi bila kichwa, ndio maana alisema
basi nitaendelea kuwa na ubavu huu.
Kwa msomaji mzuri wa Bibblia unakumbuka hadithi ya Ruthi katika
kitabu cha Ruth 1:16-17 “Naye Ruth akasema, usinisihi nikuache, nirejee
nawe, maana wewe uendako nitakwenda, nawe ukaapo nitakaa watu wako watakuwa
watu wangu, pale utakapokufa nitakufa nami, na papo hapo nitazikwa. Bwana
anitende hivyo na kuzidi, ila kufa kutatutenga wewe na mimi”
Huyo ni Ruth alipokuwa anamwambia mama mkwe wake, wakati amemsihi
aondoke kama Olpa alivyofanya. Ndugu zangu nazungumza habari za KUACHANA, siku
tulizonazo, limekuwa ni tatizo kubwa katika maisha ya wana ndoa wengi,Sio kwa
Mapadri,sio wachungaji au hata Mashekhe wasiokuwa na mlolongo wa mashauri ya
wanandoa kutaka kutengana. Na wengine maombi yao yamekwama hayajibiwi kwa
sababu ya ndoa zao. Ukisoma
kitabu cha 1Petro 3:7 kinaandika “Kadhalika nanyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, na kumpa mke
heshima, kama chombo kisicho na nguvu, na kama warithi pamoja na neema ya uzima,
kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe”
Neno linasema wazi wazi kuwa mume ukae na mke wako kwa akili.
Unaona hiyo? Kukaa na mke inatakiwa akili itumike. Je, Ni akili ya namna gani?
: Kuwa ni chombo kisicho na nguvu, japo wakati mwingine wanajitutumua kana
kwamba wana nguvu, lakini Biblia inabaki pale pale kuwa ni chombo kisicho na
nguvu, ya kwamba mume umpe mke Heshima. Kumpa heshima ni kufanyaje?
Hayo yote tuyaangalie vizuri maana ndiyo yanayoleta matatizo iwapo
mmoja atashindwa kutimiza wajibu wake. Unajua kama madereva wote wangefuata
sheria za barabarani, hakungekuwa kunatokea ajali barabarani na kama zikitokea
basi zingekuwa chache sana, pale panapotakiwa ku “keep left”, mwendo gani
unatakiwa hapo, wakati gani umpite mwezako aliye mbele, wakati gani usimame n.k!
1 Petro 3:1-6 “Kadhalika nanyi wake watiini waume zenu,
kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo
lile neno. Wakiutazama mwenendo wenu safi na wa hofu. Kujipamba kwenu kusiwe
kujipamba kwa nje, yaani kusuka nywele, na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi,
bali uwe utu wa moyoni, usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika, yaani roho
ya upole, na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu. Maana hivyo ndivyo
walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumikia Mungu, na kuwatii
waume zao,kama vile Sara alivyomtii Ibrahimu, akamwita Bwana. Nanyi ni watoto
wake, mfanyapo mema, wala hamkutishwa kwa hofu yoyote”
Itaendelea kesho..............Ungana nami tuendelee kuelimishana.
No comments:
Post a Comment