Tuesday, 20 June 2017

UMUHIMU WA MAONO (VISION) KATIKA MAISHA


Image result for VISION

Kati ya kitu ambacho hutakiwi kukosa kabisa katika maisha yako ni hali ya kuwa mtu wa maono. Maono ndio ufunguo wa pekee utakaokupa matumaini ya safari ya maisha yako ya badae ukiwa unaishi sasa. Ukiwa mwenye maono makubwa ndani yako utachunga ulimi wako usitamke kinyume na kile unachoona mbele yako. Mtu mwenye maono makubwa si mtu wa kuruhusu kuambatana na kila mtu. Mtu mwenye maono si mtu anayeweza kukata tamaa haraka kwa kuwa ni wazi anaona wapi anapotoka na wapi anakoelekea.

Huwezi kuwa na picha nzuri ya maisha yako ya badae ukakosa ujasiri kutokana na magumu unayokutana nayo njiani leo hii. Kuna nguvu kubwa katika maisha ya mtu aliyebeba maono makubwa ndani yake. Kumbuka maono ni picha halisi iliyomo moyoni mwako, inayobeba maisha yako ya badae ukiwa unaishi Sasa. Maono yanaenda na Imani. Kwa kuwa ili ufikie unachokiona ni lazima uamini ipo siku utakifikia. Na maono ndio chanzo cha hamasa (motivation) ya kweli ndani ya maisha ya mwanadamu yoyote yule.


Chanzo cha maono yoyote yale ndani ya mtu ni kutambua kusudi la kuzaliwa kwake hapa duniani. Huwezi kuwa na maono (vision) kama hujatambua upo duniani kwa kusudi gani. Siku zote unaona mafanikio juu ya kile unachokitaka katika maisha yako. Maono ni lazima yaendane na kusudi la Mungu katika maisha yako. Jifunze kuona mazuri yaliyoandaliwa na Mungu mbele yako hata kama mazingira yaliyokuzunguka hayakuruhusu uone hivyo. Kumbuka maono ndio yanayoleta shauku (desire) ya kufanikisha kile ulichokianza ndani yako.

Kusudi lako ndio linalozaa maono. Maono yanazaa malengo. Malengo yanazaa mkakati imara wa kukusaidia kufikia kusudi la maisha yako hapa duniani. Jiulize swali hili, Unaona nini katika maisha yako sasa na ya badae? Nini unachokiona ndani ya akili na moyo wako kila unapolala na kuamka? Nini kinachokupa msukumo wa kuamka mapema kabla ya wengine? Kumbuka maono ndio yanayoweza kukunyima usingizi wakati wengine wamelala, yanakufanya uwe na shauku ya kufanya kile unachoona ni fursa kwako ya kukusaidia kufikia ndoto za maisha yako.

Ni lazima uishi kulingana na maono au picha uliyonayo moyoni mwako ili kukusaidia kutimiza kusudi muhimu la maisha yako hapa duniani. Dunia imepungukiwa na watu wenye kubeba maono makubwa yanayoweza kuifanya dunia kuwa sehemu ya vile Mungu anavyotaka, hii ni kutokana na idadi kubwa ya watu wengi kuishi nje ya uwezo mkubwa (potential) walionao ndani yao. Ni wazi leo hii watu wengi wamekuwa ni wenye ndoto kubwa kwenye maisha yao lakini wameshindwa kuzichukulia hatua ndoto zao ili kuwa halisi kwa ajili ya kuwazalia matunda yatakayowapeleka kwenye ukuu.

Ukiwa mtu mwenye maono makubwa na shauku iliyojitosheleza ni rahisi sana kuleta matokeo makubwa yanayoweza kuupindua ulimwengu tunaoishi sasa. Hebu fuatilia kwa makini watu kama Bill Gates, Steve Jobs, na Mark Zuckerberg walikuwa ni watu wenye maono ya mbali kabla ya kuwa hivi tunavyowaona hii leo, na sasa wamefikia hatua ya kuupindua ulimwengu katika eneo la Teknolojia ya kompyuta na mawasiliano. Kumbe hakika inawezekana. Maono ndio dira na ufunguo wa mafanikio yako. Leo amua kuwa na maono makubwa juu ya kusudi unalolitumikia ili kukuzalia matunda yatakayokupa thamani ya pekee katika maisha yako.

Amini na inawezekana

JEROME NA ANNA

Changamoto Zinampata Mtu Anayetafuta Mafanikio Kwa Njia Ya Ujasiriamali. Soma Hapa


Kuna changamoto nyingi sana zinazompata mtu hasa pale anapoamua kujikita na kutafuta mafanikio kwa njia ya ujasiriamali; na hasa katika nchi zetu za dunia ya tatu au nchi zinazoendelea.

Lakini kwa ufupi na uchache ningependa kukupa changamoto za aina tano ambazo zimekuwa kama chachu na kikwazo kikubwa kwa wajasiriamali wengi hasa wadogo; kutofikia maono makubwa ambayo walikuwa wakitegemea kufikia katika ujasiriamali.

Changamoto ya Kwanza:

Mikopo yenye Riba Kubwa.

Jambo hili limetokea na linaendelea kutokea na kuwa sehemu ya kikwazo cha wajasiriamali wengi hasa wanaoanza biashara au kujiajiri binafsi; kushindwa kufikia malengo yao makubwa kwa sababu ya kushindwa kukopa na kuendeleza biashara zao. Hivyo makato makubwa yanayotolewa na taasisi za kifedha katika mikopo imekuwa ni kikwazo cha wajasiriamali wengi kutokuendelea kufikia mafanikio makubwa.

Hii ni mojawapo ya changamoto kubwa ambayo wajasiriamali wengi wamekumbana nayo; hasa wanapoamua kujikita katika ujasiriamali na kumiliki biashara zao binafsi.

Ninasema hili ni kwa sababu si kila mjasiriamali anaweza kujitosheleza kwa fedha zake binafsi katika kuendeleza na kukuza biashara yake binafsi hadi pale anapotaka; wapo wanaotafuta namna ya kukopa katika taasisi mbali mbali za kifedha ili kujaribu kuziinua biashara zao; lakini kikwazo kikubwa wanachokutana nacho ni riba na makato makubwa katika mikopo wanayoichukua.

Changamoto ya Pili:

Maarifa na Ujunzi wa kutosha wa kukabiliana na ushindani katika soko.

Hakuna biashara isiyopata ushindani katika soko linalotoa bidhaa au huduma zake. Kampuni ni nyingi na wajasiriamali ni wengi, hivyo kama mjasiriamali unapaswa kuingia katika soko ukiwa umejiandaa kiufahamu na kifikra ni namna gani ya kukabiliana na mazingira ya kiushindani dhidi ya washindani wako waliokutangulia au wakaokufaata nyuma yako.

Suala la kujisomea na kuongeza maarifa kila siku ni suala linalopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa kila mjasiriamali aliyeamua kuingia katika ulingo wa kibiashara, na kukabiliana na kila changamoto zote za washindani wake sokoni na nyinginezo.

Changamoto ya Tatu:

Sera za Serikali katika sekta ya Biashara na Viwanda na Sekta nyinginezo kutokukidhi uwezo wa kuwasaidia wajasiriamali wadogo.

Zipo sera mbali mbali katika nchi yetu na hata katika nchi nyingine zinazoendelea, ambazo zimekuwa ni changamoto kubwa kwa wajasiriamali wengi kushindwa kufikia mafanikio katika biashara zao.

Mifano kadhaa ya mambo yanayowakwamisha wajasiriamali wengi ni juu ya usimamizi mbaya uliopo juu ya makato ya kodi (Kodi ni lazima); ila kodi inayowapa nafasi ya kuwasaidia wajasiriamali kuiona kesho ya biashara zao; na si kuzuia biashara hizo kukua.

Taasisi za mamlaka ya ubora wa viwango vya bidhaa na vyakula kutokuwa na usimamizi mzuri katika kuwaelimisha na kuwaweka sawa wajasiriamali wadogo kutambua nafasi ya kuzalisha bidhaa katika ubora wanaoutaka. Hivyo taasisi hizi zimegeuka chachu kwao na kuwa sehemu ya kuwarudisha nyuma wajasiriamali wadogo wanaotaka kufanikiwa kupitia ujasiriamali.

Changamoto ya Nne:

Mtazamo wa Wanaokuzunguka.

Bado kuna tatizo kubwa katika nchi zetu zinazoendelea; kuwepo kwa ubinafsi, husuda na mtazamo mbaya wa kunyanyuana na kusaidiana kimaisha; jambo hili limekuwa kama sehemu ya kurudishana nyuma kwa wajasiriamali wengi na kushindwa kufikia mafanikio makubwa.

Haya yote ni changamoto kubwa kwa mjasiriamali mdogo hasa kwa yule anayeanza kuingia sokoni kwa mara ya kwanza. Wajasiriamali waliokomaa katika soko ni vizuri kutoa machango wao wa kutosha katika kuwasaidia wajasiriamali wadogo kuendelea, na si kuwakwepa.

Changamoto ya Tano:

Kuruhusu Matatizo binafsi kuwa sehemu ya pili ya biashara yako.

Kama kuna jambo linalowafanya wajasiriamali wengi kukwama kibiashara na linaloweza kuwa changamoto hata kwa wale wanaotaka kuwa wajasiriamali kunzia sasa. Ni juu ya kukubali na kuruhusu matatizo binafsi kama vile ya kifedha, kiuchumi na kifamilia kuwa sehemu ya biashara zao.

Kuchanganya masuala binafsi ya kifedha na kifamilia katika biashara yako ni mwanzo pekee wa kutosha kuiangamiza biashara yako milele, na kusababisha kutokufikia mafanikio makubwa uliyotamani kuyafikia kama mjasiriamali.

Hizo ni baadhi ya changamoto kubwa tano ambazo zimekuwa mtihani mkubwa kwa wajasiriamali wengi; kutokufikia mafanikio yao ya ujasiriamali hasa katika kupiga hatua kubwa na ya juu ya kibiashara.

Zipo changamoto nyingine nyingi zaidi; ila kwa kupitia changamoto hizo kuu, nadhani utakuwa umenielewa na zaidi umejifunza jambo la kipekee na sasa kazi ni yako kuchukua hatua ya kukabiliana nazo kama unataka kuingia katika ujasiriamali au tayari wewe ni mjasiariamali.

Kumbuka changamoto yoyote ile ni fursa ya kuleta maendeleo; unaweza kufanikiwa katikati ya changamoto unayoiona kama ni kikwazo cha wewe kutokufikia mafanikio makubwa katika biashara yako.

Hadi kufikia hapo nakutakia Mafanikio mema yenye baraka na nguvu zaidi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

JEROME NA ANNA

Sunday, 18 June 2017

HOFU YA MUNGU IWE CHACHU YA KUTAFUTA MCHUMBA



Ndoa ni jambo la kiroho wala sio kimwili.
Ukitaka ndoa kwako liwe jambo la kimwili chunga sana maana unaweza ukawa umedandia mtumbwi uliotoboka, uko baharini na nchi kavu haionekani iliko.
Changamoto kubwa ni jinsi ya kumpata mwenzi sahihi wa kukufaa ili mfunge naye ndoa na kuendelea na maisha ya ndoa kwa uzuri, furaha na amani.

Image result for ndoa
Mithali 31:10 '' Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani.''

Mke mwema au mume mwema ni nani awezaye kumwona?
Huo ndio mtihani mkubwa lakini ukweli ni kwamba kwa maombi na utakatifu hakika utamjua tu mke mwema wako au mume mwema wako.

Mwanzo 2:21-24 '' Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu BWANA Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.''


Haikumsumbua Adamu kumjua Mkewe baada ya Mungu kumletea. Lakini leo Akina Adamu wengi Mungu akiwaletea Eva wao huwa wanakataa kwa sababu ya mambo ya kidunia yaliyopotoshwa na shetani.
Unakuta kijana anataka binti mrefu mweupe msomi na asiwe muongeaji sana. Hayo ni mambo ya kidunia yaliyopindishwa na shetani ndio maana wengi huacha kuwapata walio katika kusudi la Mungu bali hupata walio katika akili zao tu. Unaweza ukampata msomi kweli na mzuri wa sura lakini kwa malezi yake tu katika familia yao hafai kuwa mke mwema maana hajui majukumu ya mwanamke na wala haheshimu ndoa.

Adamu alimjua Eva wake kwa sababu ya kuishi maisha matakatifu ya bila dhambi.
Akina Adamu wa leo wengi wako katika vifungo vingi ambavyo vingine ni vifungo vya kuwazuia kuoa. Leo akina Eva wengi hadi wanaolewa walishaingia katika maagano ya kipepo hata mengi kuliko umri wao.
Leo hata marafiki sio wote ni wema maana rafiki anaweza akamwendea kwa mganga rafiki yake ili tu huyo rafiki asiolewe kabla yake.
Sasa Kama huyo mwenda kwa mganga hataolewa kwa wakati basi na rafiki yake hataolewa, ni hatari.Dunia imeharibika sana na kwa jinsi hiyo ni Bwana YESU KRISTO tu anayeweza kutukomboa na kutuokoa na kutufanya tukarudi katika asili yetu aliyotuumbia MUNGU Muumbaji wengi.
Suala la ndoa leo linahitaji umakini sana na umakini namba moja ni kumpata Mume/mke mcha MUNGU mwenye hofu ya MUNGU, ukikosea hapo tu hakika utakuwa umewaolea wajamaa au umeolewa na mume wa watu na sio wako peke yako, ni hatari mbaya sana sana.
Ndoa chanzo chake kinatakiwa kiwe rohoni na sio mwilini.
Wanaotaka Kuoa/kuolewa Wengi Husema Wanahitaji Mchumba Mwenye Hofu Ya MUNGU. 
Ni Vizuri, Lakini Kwanza Hakikisha Wewe Una Hofu Ya MUNGU Ndipo Umuhitaji Mchumba Mwenye Hofu Ya MUNGU. 
Sio Wewe Huna Hofu Ya MUNGU Kisha Unataka Mwenye Hofu Ya MUNGU. 
Yakobo 4:7-10 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za BWANA, naye atawakuza.''
Kumtii MUNGU ni jukumu la kila mwanadamu.
Jukumu la kumtii MUNGU ni la muoaji na muolewaji, ni la kila mtu.
Huwezi ukataka tu mwenye hofu ya MUNGU huku wewe hata hujui hofu ya MUNGU ina umuhimu gani katika maisha yako binafsi kwanza. 
Haviendani Hata Kidogo, Na Dalili Moja Ndogo Ya Mtu Kutokuwa Na Hofu Ya MUNGU Ni Kutokutoa Fungu La Kumi, Dalili Nyingine Ni Kutaka Ngono Wakati Wa Uchumba, Dalili Nyingine Ni Kutokudhuria Ibada Na Dalili Kuu Ni Dhambi. 
Je, Wewe Una Hofu Ya MUNGU Hata Uwe Na Haki Ya Kumpata Mchumba Mwenye Hofu Ya MUNGU?
Tafakari maandiko haya ili uone utu mwema ulivyo na faida. 
Mithali 13:15-21 ''Ufahamu mwema huleta upendeleo; Bali njia ya haini huparuza. Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa; Bali mpumbavu hueneza upumbavu. Mjumbe mbaya huanguka maovuni; Bali mjumbe mwaminifu ni afya. Umaskini na fedheha zitampata yeye akataaye kurudiwa; Bali yeye aangaliaye maonyo ataheshimiwa. Haja iliyopatikana ni tamu nafsini mwa mtu; Bali kujitenga na maovu ni chukizo kwa wapumbavu. Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia. Uovu huwaandamia wenye dhambi; Bali mwenye haki atalipwa mema.'' 
Ufahamu mwema huleta upendeleo, ufahamu mwema ni kumcha MUNGU, Je una mcha MUNGU hata upendelewe kwa kupewa mtu sahihi mwenye ufahamu mwema kama wako?
Mwenye busara hutenda kazi kwa maarifa, Busara njema ni busara inayoongozwa na Neno la MUNGU. Wasio na busara ndio hutaka ngono wakati wa uchumba.
Enenda na wenye hekima nawe utakuwa na mwenye hekima, hekima kuu ni Neno la MUNGU.
Wengi huenda na wadhambi ndio maana baada ya kuoa au kuolewa huacha hata kuhudhuria ibada kanisani.

Wanandoa wengi walioanza vibaya katika ndoa zao ndio hao hawaaminiani na ndio hao ni migogoro kila siku na ndio hao hata uvumulivu ni hakuna katika ndoa zao.Mfano Kuna wanawake wengine kwenye ndoa akisemwa kidogo tu juu ya kuzidisha chumvi kwenye mboga yeye anafungasha nguo na vyombo tayari kwenda kwao. Hadi mumewe amfuate kwao basi kielelezo cha ndoa takatifu kinakuwa kilishapotea siku nyingi
Kuna wababa wako busy kuvisifia vibinti mitaani ndio maana ndoa zao hazijawahi kuwa vielelezo. Mkeo una miaka 3 hujawahi kumsifia lakini vibinti unavisifia kila siku.
Mbaya sana hiyo.

Kuna wanandoa kupigana busu hadi waambiwe na daktari
Kuna wanandoa hupendana wakiwa kanisani tu lakini nje ya kanisa kila Mtu mbabe.
Maombi kwenye ndoa ni muhimu.
Haki sawa za Beijing Nazo haziko kibiblia ndio maana zinasababisha kielelezo kutoweka kwenye ndoa nyingi.

Waebrania 13:4-5 ''Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu.Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. ''
Ndugu uliye katika ndoa na wewe ndugu unayetarajia kuingia katika ndoa nakushauri haya yafuatayo;
Usikubali shetani akautumia moyo wako.
Usikubali shetani akautumia mwili wako.
Usikubali shetani akakitumia kinywa chako.
Usikubali shetani akayatumia mawazo yako.
shetani siku zote kazi zake ni kuhakikisha huendi uzima wa milele.
Ukimwazima kitu chako shetani atakupeleka kubaya.
Kataa kutumiwa na shetani maisha yako yote.

1 Petro 5:6-11 '' Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa MUNGU ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani. Na MUNGU wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika KRISTO, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu. Uweza una yeye hata milele na milele. Amina.'' 


Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

JEROME NA ANNA

Changamoto za Mwanaume Kuoa Mwanamke Aliyemzidi Miaka Mingi:

Jamii nyingi za kiafrika huamini kwamba siku zote mwanamke ni lazima awe na miaka michache kuliko mume wake. 

i. Maneno maneno ya kuvunja moyo kutoka kwa jamii
Inapotokea mwanamke akawa na miaka mingi sana kuliko mumewe jamii huweza kuongea maneno ambayo wakati mwingine huwakosesha raha na amani. Unapogundua watu kila ukipita wanakusema wewe na kukusema kwenyewe ni kukusema vibaya sio kukusema kwa mema hilo jambo huumiza sana moyo wa mtu na kumfanya kuamini kwamba kila wakati watu watakuwa wakimsema yeye hata wakati ambapo watu watakuwa wakiongelea mambo mengine yeye atajihisi tu kuwa wanamsema yeye. Kadri miaka inavyozidi kwenda mmoja anaweza kuona vibaya kuongozana na mwenzake kutokana na hayo maneno ya watu wa nje kwamba hawaendani na kwamba ameoa mwanamke mzee au ameolewa na mwanaume mzee au wengine kumshambulia mwanamke kuwa ameolewa na mwanaume mdogo au mtoto hali hii huchangia kupunguza uhuru wa kimahusiano kati ya wanandoa hawa hasa mbele za jamii. Baadhi ya watu katika jamii wanaweza kuongea juu yao mambo ambayo yatawaumiza sana mioyo yao.

ii. Kukosa Uhuru wa kuwa na Mwenzi wako Hadharani.
Kutokana na maneno ya watu mitaani, kanisani, kazini na kwingineko mnaweza kukosa uhuru wa kuongazana pamoja au kumtambulisha kwa marafiki au inapotokea mmealikwa kwenye sherehe au hafla fulani unapata utata wa kuongozana kutokana na kuhofia kunyooshewa vidole na watu kwa kuwasema vibaya.

iii. Kupishana kwa mapendeleo na maslahi “Hobbies & Interests" Baina ya Wanandoa Hao
Moja ya changamoto inayowakabiri wanandoa ambao wamepishana umri wa miaka mingi ni kwamba mmoja atakuwa anaishi kwenye ulimwengu wa kiujana na mwingine atakuwa anaishi kwenye ulimwengu wa Kiutuuzima au ulimwengu wa uzee. Tatizo litakalotokea hapa kila mmoja anajaribu kumvuta mwenzake kwenye ulimwengu wake. Yule ambaye ni kijana atakuwa anajaribu kumvuta yule mtu mzima au mzee kwake kwa maana kwamba yeye kama kijana hataki kufanya mambo ya kizee anataka kwenda na wakati kwa kufanya mambo ya kiujana ujana. Wakati naye yule mzee atakuwa akimvuta kijana kwake kwamaana kwamba yeye kama mtu mzima au mzee hawezi kufanya mambo ya kitoto kwani hata watu wakisikia anafanya hivyo wataweza kumuuliza kwamba wewe mtu mzima bado unafanya mambo ya vijana!? Kwahiyo kutakuwa na vuta nikuvute ambayo itasababisha mmoja kuona kwamba huyu mtu naona haikuwa chaguo sahihi maana ananitesa badala ya kunifanya nifurahie maisha ya ndoa.

iv. Changamoto ya Kutoendana na Kuangalia Nje ya "Fance"
Kadri miaka itakavyozidi kwenda ile "gap" ya umri itakuwa ikijitokeza kwa ukubwa zaidi. Kijana ataanza kuona huyu mzee hatuendani namimi yupo nyuma ya wakati na kuanza kuvutiwa zaidi na mtu mwingine wa rika lake. Mfano kama kijana ameoa mwanamke ambaye wamepishana sana umri, kijana anaweza kutamani mkewe awe anavaa yale mavazi ya ujana ambayo huvaliwa na wasichana mitindo na mishono ya kiujana ili atakapokutana na marafiki zake waone kuwa ana mwanamke ambaye anakwenda na wakati. Kwa upande wake huyo mwanamke kulinganana umri wake hawezi kuthubutu kuvaa mavazi ya kiujana kama hayo na hapo mgogoro huweza kutokea na wote wawili kuona kuwa hawaendani kabisa.

v. Imani ya kwamba Ndoa ni Kwajili ya Kupata Watoto
Katika tamaduni na mazingira yetu ya Kiafrika, umri wa mwanamke anapoolewa ni wamsingi sana hasa linapokuja swala la kuzaa watoto. Kwa tamaduni za kiafrika swala la kuzaa watoto katika ndoa ni jambo la msingi sana kwa jamii nyingi za kiafrika. Kwahiyo mwanaume anapooa anakuwa na mategemeo kwa sehemu kubwa kwamba atapata watoto kupitia mke ambaye anamuoa.

vi. Jamii Huamini kwamba Mwanamke Mwenye Umri Mkubwa Atashindwa Kuzaa.
Jamii nyingi huamini kwamba kuoa mwanamke mwenye umri mkubwa anaweza kushindwa kumzalia watoto mumewe.
Kulingaana na watafiti wanasema kwamba kadri mwanamke anavyoziku kuongezeka umri ndivyo ambavyo viungo vyake vya uzazi hupoteza uwezo wake wa kushika mimba na kuzaa watoto.

vii. Kiwango Muafaka cha Kupishana Umri Kati ya Mwanamke na Mwanaume.
Kwa Mwanaume: Inashauriwa kwamba kwa mwanaume miaka 5 hadi 10 inafaa kupishana kati ya mwanaume na mwanamke anayetarajia kumuoa. Kwamaana ya kwamba mwanaume anaweza kuoa mwanamke ambaye yeye mwanaume anakuwa amemzidi huyo mwanamke miaka miwili, mitano hadi 10.

Kwa Mwanamke:

viii. Inashauriwa pia kwa mwanamke kuzidi miaka miwili hadi 5 kwa mwanaume anayetarajia kuolewa naye. Hii inamaanisha kwamba mwanamke akimzidi mchumba wake au mume wake miaka miwili hadi mitano itakuwa ni sawa hakutakuwa na tofauti kubwa sana wala madhara makubwa.

ix. Kuna Athari kwa wanandoa wakipishaza zaidi ya miaka 10.
Wanandoa wanapokuwa wamepishana kwa zaidi ya miaka 10 kunakuwa na utafauti mkubwa katika kuhusiana kwao kama jinsi tulivyoelezea hapo juu.

x. Ushauri kwa Wachumba Waliopishana Umri Mkubwa
Wachumba ambao wana tofauti kubwa ya umri wao, wanashauriwa kutafuta ushauri kwa washauri wazuri (good counselors) kabla ya kuoana. Hata hivyo bado Mungu ni wa neema na miujiza anaweza akatenda hata kwa mwanamke au mwanaume mwenye umri mkubwa kuliko mwenzake hata kama ameshapitisha muda wa kuzaa au na mambo mengine Bwana bado hashindwi.
Luka 1:37 
Kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.
Wafilipi 4:13 
Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

JEROME NA ANNA

Featured post

MWANAMKE YAFUATE HAYA; NI MUHIMU KWA MAHUSIANO YAKO

1. Degree yako ya fist class uliyoipata chuo kikuu haiwezi kukufanya uwe mke first class katika ndoa yako bali ni heshima yako na uthubu...