Thursday, 25 February 2016

KUNA UBAYA GANI KUISHI PAMOJA KABLA YA KUOANA?


Kuna wakati fulani niliamua kwenda dukani pale mijini Dodoma katika duka la mfanyabiashara mmoja maarufu sana.Lengo la kwenda pale lilikuwa kununua nguo(suti).Sasa mimi niliamua kununua suti manake kulikuwa na sherehe maalumu sana nilikuwa nimealikwa na mmoja wa rafiki zangu nyumbani kwa mbunge mmoja pale area D.Mimi kwa kuwa nilijua suruali navaa kiuno namba fulani,basi sikuhangaika kujipima ile suti.Iliangaliwa tu kwa nje na baada ya kuona namba ya suruali basi nikanunua.Kwa bahati mbaya mimi huwa napenda nikinunua vitu nipewe na risiti.Nilipewa risiti na kuondoka dukani.Kufika chuoni sikujaribu ile suti hadi siku ya jumamosi nilipomaliza kuoga ndio nikafungua mfuko na kuvaa suti.Cha kushangaza suti ile ilikuwa kubwa sana kwangu.Suruali ilikuwa imezidi inchi tano kiunoni na pia ilikuwa ndefu sana.Pia lile koti la suti lilikuwa pana kuliko mimi na mikono yake ni mirefu kiasi cha kufunika kabisa mikono yangu.Nisingeweza kuirudisha dukani kwa kuwa risiti iliandikwa maneno “Goods once sold are not returned).kwa maana hiyo nilijifunza kuwa sitanunua tena nguo yoyote bila kuijaribisha kama inanikaa na kama nikivaa napendeza.Labda nianze kwa kukuuliza ndugu msomaji wangu,je? Wewe unaweza kununua nguo bila kuijaribu?Naamini jibu litakuwa ni hapana.Lazima uijaribu kwanza.
Watu wengi hupenda hutumia mfano huo kuhusu ndoa. Wanaona ni afadhali mwanamume na mwanamke kuishi pamoja kabla ya kuoana kisheria. Wao wanasema ‘mambo yakienda mrama, wanaweza kutengana bila kukabiliana na matatizo ya talaka kwa kuwa eti Masuala ya talaka yanayogharimu sana.
Inawezekana  baadhi ya wale walio na maoni kama hayo wamemwona rafiki yao aliyefunga ndoa akivumilia ndoa mbaya. Au huenda wengine wakawa wamejionea hali mbaya za ndoa ambayo mume na mke hawapendani tena. Kwa sababu hiyo, huenda wakaona kuishi pamoja bila kufunga ndoa kuwa jambo lenye hekima ili kuzuia matatizo ya baadaye,au wakaamua kuishi pamoja kwanza ili kusomana tabia zao.
Biblia ina maoni gani kuhusu jambo hilo? Ili kupata  majibu sahaihi, tunahitaji kuchunguza kile ambacho Neno la Mungu linasema kuhusu ndoa.


“Mwili Mmoja”
Biblia inaheshimu sana ndoa, na hilo halishangazi kwa kuwa mpango wa ndoa uliidhinishwa na kuanzishwa na  Mungu mwenyewe. (Mwanzo 2:21-24) Tangu kuumbwa ulimwengu, Mungu alikusudia kwamba ndoa iwaunganishe mwanamume na mwanamke kuwa “mwili mmoja.” (Mwanzo 2:24) Baada ya kunukuu maandiko matakatifu ya Biblia kuhusu jambo hili, Yesu aliongezea hivi: “Kile ambacho Mungu ameunganisha mtu yeyote asikitenganishe.”—Mathayo 19:6.
Ni kweli kwamba wengine ambao hufunga ndoa baadaye hupeana talaka(Baada ya kuishi pamoja muda mrefu). Watu hawatalikiani kwa sababu kuna tatizo na mpango wenyewe wa ndoa; badala yake wanatalikiana kwa sababu mwenzi mmoja au wote wawili walishindwa kuheshimu kiapo walichotoa siku ya arusi yao.
Kwa mfano: Tuseme mwanamume na mwanamke wana gari, lakini hawalitumii kulingana na maagizo yaliyotolewa na mtengenezaji wake. Nani atalaumiwa gari hilo linapoharibika? Je, ni mtengenezaji au ni wenye gari ambao walishindwa kulitumia kutokana na maelekezo ya mtengenezaji?
Kanuni hiyohiyo inahusu ndoa. Mume na mke wanapodumisha uhusiano wao na wanajitahidi kutatua matatizo yao kwa kutumia kanuni za Biblia, si rahisi watalikiane. Wanajihisi wakiwa salama katika ndoa ile kwa kuwa kila mmoja anawajibika kwa mwenzake. Kwa sababu hiyo ndoa inakuwa msingi wa uhusiano wenye upendo.Na inafikia hata hatua ya kuwa na damu za aina moja.Jiulize kwanini watu wakioana na wakaishi kwa upendo ukiwatazama sura zao ni kama zinafanana?
“Mjiepushe na Uasherati”
Lakini bado huenda wengine wakajiuliza: ‘Kwa nini basi tusiishi pamoja kwanza? Je, kujaribu uhusiano huo kabla ya kuanza kuwajibika si kunaonyesha kwamba tunaiona ndoa kuwa takatifu?’
Biblia inatoa jibu la wazi. Paulo aliandika: “Mjiepushe na uasherati.” (1 Wathesalonike 4:3) Neno “uasherati” linamaanisha mahusiano yote ya ngono nje ya ndoa. Hilo linahusisha ngono kati ya watu wawili wanaoishi pamoja, hata kama wanakusudia kuoana. Kulingana na maandiko matakatifu, basi ni kosa kwa watu wawili kuishi pamoja kama mume na mke hata ikiwa nia yao ni kuoana baadaye.
Kwa bahati mbaya vijana wengi kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia yaliyopelekea kubadilika mfumo wa maisha wanadhani maadiko hayo yamepitwa na wakati. Isitoshe, katika nchi nyingi, ni jambo la kawaida kwa watu kuishi pamoja—iwe wanakusudia kuoana au la, na mahali pengine watu wanaishi kwa mkataba kabisa. Lakini fikiria matokeo ake ni yepi hasa?. Je, wale wanaoishi pamoja wamepata mafanikio katika familia hiyo? Je, wana furaha kuliko wale waliofunga ndoa? Je, tarakimu zinaonyesha kwamba wenzi wa ndoa walioishi pamoja kabla ya kuoana ni waaminifu kuliko wale wengine? Uchunguzi unaonyesha matokeo tofauti kabisa. Kwa kweli, imeonekana kwamba wenzi wa ndoa walioishi pamoja kabla ya kufunga ndoa wana matatizo mengi zaidi ya ndoa na mwishowe hutalikiana.Maana yake ni kwamba hakuna uhusiano wa karibu na ulio wa afya kati ya kuishi pamoja kabla ya ndoa na mafanikio baada ya kufunga ndoa hiyo.
Wataalamu toka Ireland wanasema kwamba uchunguzi kama huo una kasoro. “Watu wanaoamua kufunga ndoa bila [kuishi pamoja] kwanza wana mtazamo tofauti kabisa na watu wanaoamua [kuishi pamoja] kwanza,” anaandika mtaalamu mmoja wa saikolojia. Anasema kwamba jambo kuu si kuishi pamoja; badala yake jambo kuu ni “kuthamini ile hali ya kuoana.”
Hata ikiwa hilo ni kweli, linakazia tu umuhimu wa kusitawisha maoni ya Mungu kuhusu ndoa. Biblia inasema: “Ndoa na iheshimiwe na watu wote.” (Waebrania 13:4) Mwanamume na mwanamke wanapoapa  kuwa mwili mmoja na kuheshimu mpango wa ndoa, wanakuwa na kifungo kisichoweza kukatwa kwa urahisi.—Mhubiri 4:12.

Kwa hiyo, tukirudi katika mfano wa kwanza, ni jambo linaloingia akilini kujaribu suti au vazi kabla ya kulinunua. Hata hivyo, wazo hilo haliungi mkono kuishi pamoja kabla ya ndoa. Badala yake, mtu anapaswa kutumia muda kumfahamu yule anayekusudia kumuoa au kuolewa naye. Hiyo ni hatua muhimu ambayo mara nyingi hupuuzwa lakini ni moja kati ya siri za kufanikiwa kwa familia na kuwa na ndoa yenye amani na furaha wakati wote.
Biblia imeweka mkazo na kusisitiza tendo la ndoa kati ya waliooana tu-Zaburi 84:11;1 Wakorintho 6:18.Kwa hiyo wanaoishi pamoja kabla ya kuoana/ndoa wanavunja amri hii ya Mungu na wanamchukiza ungu kwa kuwa wanalala na kufanya ngono kama mume na mke kabla ya kuwa na agano halaliyaani ndoa.

Kuishi pamoja kabla ya kufunga ndoa hakutoi nafasi ya nyie kusomana…la hasha.Pale mnaisho tayari kama mme na mke japo kwa wizi.Biblia imeainisha njia bora na vigezo vya wazi vya namna ya kumsoma mwenza wako wa maisha mkiwa hamuishi pamoja-Rejea…..Ruthu 1:16, 17; Methali 31:10-31. Biblia inasema: “Yeye aliye na mazoea ya kufanya uasherati anautendea dhambi mwili wake mwenyewe.” (1 Wakorintho 6:18) Katika miaka ya karibuni, ukweli wa maneno hayo umeonekana kwa sababu ya mamilioni ya watu ambao wamekufa kutokana na UKIMWI na magonjwa mengine ya zinaa. Lakini si hilo tu. Uchunguzi umeonyesha kwamba ni jambo la kawaida kwa vijana wanaofanya ngono kushuka moyo sana na hata kujaribu kujiua. Pia, ukosefu wa maadili husababisha mimba zisizotakiwa, na hilo hutokeza katika visa fulani kishawishi cha kutoa mimba. Kwa kufikiria mambo hakika, tunaweza kukata kauli kwamba sheria ya maadili iliyo katika Biblia haijapitwa na wakati.

 Hujachelewa,Mlango bado iko wazi kutubu na kujisahihisha.
Endelea kunifuatilia kupitia bLOG hii ujipatie maarifa zaidi
Karibu sana!!

No comments:

Post a Comment

Featured post

MWANAMKE YAFUATE HAYA; NI MUHIMU KWA MAHUSIANO YAKO

1. Degree yako ya fist class uliyoipata chuo kikuu haiwezi kukufanya uwe mke first class katika ndoa yako bali ni heshima yako na uthubu...