EPUKA MAMBO HAYA, YATAKUVUNJIA HESHIMA KATIKA JAMII
1. UGOMVI
Ikiwa wewe ni mtu mgomvi kila jambo dogo linalotokea wewe wakurupuka na kuanzisha ugomvi hakika jamii itakudharau mno, jifunze kutumia busara na hekima kupitia mazungumzo katika kutatua migogoro au sintofahamu katika jamii unayoishi utaheshimika mno.
2. KUJITENGA
Iwapo unakuwa mtu wa kujitenga na jamii, hushiriki misiba wala sherehe na majirani, umejifungia getini kwako ukitoka asubuhi kurudi usiku uko busy na kazi huna hata siku moja ya kuwa tembelea kuwasalimu majirani n. k jua jamii itakutazama kama mtu mbinafsi mwenye dharau, kiburi, jeuri, majivuno, nyodo na roho mbaya hivyo ni vema kuishi na watu wote vizuri tenga japo mda wa kuwasalimu na kuwajulia hali majirani pia usisahau kushiriki matukio na shughuli za kijamii ikiwemo misiba, sherehe, michezo, matamasha n. k
3. UMBEA NA UONGO
kila jambo unalosikia sio kulisambaza kama huna uhakika nalo na hata kama una uhakika nalo usilisambaze kama hujapewa kazi hiyo hapa namaanisha epuka umbea, pia epuka kuzusha mambo ya uongo ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima katika jamii. Mtu mmbea na muongo hudharaulika sana katika jamii na huwa haaminiki hata pale anapokua na hoja ya msingi.
4. MUONEKANO.
. Muonekano ninaouzungumzia hapa ni usafi wa mavazi na mwili kwa ujumla. Hata siku moja hakuna mchafu anayeheshimika katika jamii anayoishi hata kama ana kipaji kikubwa kiasi gani.
Kwa hiyo uchafu wa mavazi na mwili huchangia mtu kudharauliwa katika jamii anayoishi.
Linaweza kuwa jambo dogo sana lakini ni moja kati ya sababu kubwa inayochangia kuporomoka kwa thamani yako mbele ya wenzako.
5. MAZUNGUMZO.
Hapa naomba nieleweke kuwa unachokizungumza kinaweza kukujengea heshima au kukubomolea heshima. Kauli zisizo na busara zitakufanya udharaulike kwa kila mtu. Uropokaji usiokuwa na mantiki huchangia kuporomosha heshima yako hasa kama utakuwa muongeaji zaidi.
6. UTENDAJI WAKO WA KAZI.
Ndugu zangu, siku zote heshima ya mtu ni kazi. Watu wengi hawapendi kufanya kazi kwa bidii huku wengine wakijiendekeza kwa tabia ya kuombaomba, jambo hilo halifai kwa vile huchangia kubomoa heshima yako mbele ya jamii. Fanya kazi usiishi bila kujishughulisha.
7. KUTOTIMIZA AHADI.
Kama una tabia za kuahidi mambo halafu unashindwa kuyatekeleza, basi unajiweka katika nafasi mbaya ya kutunza heshima yako katika jamii unayoishi. Bora ukwepe kutoa ahadi kuliko kuahidi na kutotimiza.
8. SIFA ZISIZO NA MAANA.
kuna msemo ambao unasema kwamba: “Ukitafuta heshima kwa gharama ya juu, basi utalipwa dharau kwa bei nafuu.”
Msemo huu unamaanisha nini? Siku zote ukiwa unafanya mambo yako kwa ajili ya kusifiwa au mazungumzo yako kuwa ya kujiinua, watu watakudharau.
9. KUTOKUWA MWAMINIFU.
Suala la uaminifu ni pana, kuna uaminifu wa fedha, siri, dhamana na mambo kama hayo, hivyo ni vema kila unachoaminiwa lazima ukitunze kwani ukiwa mtu wa kuvunja uaminifu fahamu kuwa utashusha heshima yako.
10. KUTOKUSALI
Iwapo unaishi kama fisi hujulikani ni muislamu au mkristo, hujulikani unasali msikitini au kanisani basi tambua heshima yako kwenye jamii itashuka mno maana watakua na shaka kuhusu maadili na utashi wako, jamii iliyostaarabika huwa na watu wacha Mungu ambao huzingatia vipaumbele vya dini ikiwemo upendo, ushirikiano, umoja, kusaidiana na kuishi kama ndugu. Sasa wewe ndugu hueleweki upo upo tu unafikiri wanaokuzunguka watakuelewaje kama sio kukuhisi wewe ni muhuni, mchawi, mwizi, malaya, kahaba, fisadi, tapeli, kicheche, freemason n. k?
11. UHUNI/UMALAYA
Hizi ni tabia mbaya sana ambazo huweza kukuvunjia heshima kwa kiasi kikubwa katika jamii, tabia za uhuni, umalaya, ukahaba, usaliti na michepuko ni vyanzo vikuu vya ueneaji wa magonjwa ya zinaa ikiwemo ukimwi pia mimba zisizotarajiwa na hatimaye ongezeko kubwa la watoto wa mitaani. Tabia hizi pia hupelekea uvunjikaji wa ndoa nyingi, mafumanizi na hata mauaji.
Endelea kuelimika kupitia nachocharuwa.blogspot.com naikikupendeza mshirikishe mwenzako kwa kushare blog address.
No comments:
Post a Comment