JINSI YA KUWEKA VIPAUMBELE KATIKA MALENGO HADI KUYAFIKIA
Kila mtu ili kuweza kufikia mafanikio ni muhimu kwake kujiwekea malengo. Malengo haya anayojiwekea huwa ni lazima kuyatimiza. Inapofika mahali ukawa ni mtu wa kushindwa kutimiza malengo yako mara kwa mara, hiyo inakuwa ni hatari na shida kwako kuelekea kwenye safari ya mafanikio. Jaribu kujiuliza pale unapokuwa hutimizi malengo yako huwa unajisikiaje? Bila shaka ni vibaya.
Lakini hata hivyo pamoja na kujiwekea malengo hayo kuna wakati huwa tunajikuta tunakuwa tunamalengo mengi ambayo huanza kutuchanganya na kushindwa kujua tufanye lipi kwanza na tuache lipi. Kwa mfano, katika hali ya kawaida unaweza ukajikuta una malengo mengi zaidi ambayo umepanga na unatakiwa kuyatekeleza, hapo unafanyaje?
Kwa kawaida malengo yanapokuwa mengi unakuwa huna uwezo wa kuyatekeleza yote kwa pamoja hata ungefanyaje?
Hii yote huwa inatokea hivyo kwa sababu, kila lengo linakuwa linachukua muda na nguvu kulitekeleza hadi kufanikiwa. Hivyo malengo yanapokuwa mengi inakuwa siyo rahisi kufanikiwa kutokana na sababu hiyo.
Kwa lugha nyingine hapo katika uwekaji wa vipaumbele chagua kile kilicho cha muhimu kuliko vingine vyote anza kukitekeleza. Kitu hicho kikishakamilika nenda kingine tena. Kwa kufanya hivyo utajikuta malengo yako yanatimia moja baada ya jingine na mwisho wa siku utajikuta malengo yote yametimia. Acha kubabaika na uzuri wa malengo mengine, ukishaweka kipaumbele, fata lengo moja tu, mpaka litimie.
Acha kujifanya kutekeleza malengo yote kwa wakati mmoja hutaweza na itafika mahali lazima utakwama tu.
Nguvu yako kubwa ya kukufanikisha hasa pale unapokuwa na malengo mengi ni kufanya lengo moja moja kwanza. Hiyo ndiyo siri ya ushindi ilioyopo katika uwekaji wa vipaumbele.
Hivyo, watu ambao wataweza kuyapa vipaumbele malengo yao. Katika maana halisi na mtiririko mzuri ni wazi kuwa lazima watafanikiwa. Chukua hatua hii ya kuweka vipaumbele katika malengo yako ili ufanikishe, kufaulu na kusonga mbele kwa ujasiri. Tegemea mafanikio makubwa kama utatekeleza hili.
Endelea kufuatilia blog hii kupata elimu juu ya Mambo mbalimbali yenye maslahi kwako na jamii yako,usisahau kushirikisha wengine!!

No comments:
Post a Comment