Vijana wengi wamejikuta wakiitwa
wahuni kutokana na kuwa na uhusiano wa kimapenzi na makundi ya wanaume au
wanawake. Hata hivyo wachunguzi wa masuala ya mapenzi wanasema idadi kubwa ya
wapenzi si kigezo sahihi cha kupima tabia ya mtu na kumhusisha na uhuni.
Watalaam hao wanataja safari ya
kupata chaguo halisi la mwanaume/mwanamke wa maisha ndiyo inayowaponza wengi
kiasi cha kujikuta wameingia katika kashfa ya kuwa na uhusiano na dazeni ya
wapenzi.
Wanasema msichana/mvulana
anayeingia katika uwanja wa mapenzi kwa kuwa na hisia za kufanya ngono, hukosa
umakini wa nani anafaa kuwa mpenzi wake kutokana na kukosa elimu ya uhusiano
kutoka kwa wazazi wake.
Kwa mantiki hiyo, bila upembuzi
wa kina, mtu asiye na elimu ya jinsi ya kumpata mpenzi wa kweli hujikuta
ameangukia kwa mwanaume/mwanamke asiyemfaa, ambapo baadaye huamua kuachana na
huyo na kwenda kwa mwingine kujaribu bahati tena ya kupata penzi la kweli.
Zinatajwa zawadi, hitaji la
kusaidiwa kimaisha, mvuto wa kimahaba na mazoea kuwa ni vichocheo
vinavyowaangusha wengi kwenye mapenzi na wasiowafaa.
Ukweli ni kwamba mtu aliyenaswa
kwa ‘ujinga’, huwa hakatwi kiu ya penzi na mwanaume/mwanamke asiye chaguo
sahihi la maisha yake. Hivyo hufikia maamuzi ya kujiingiza katika uhusiano mpya
mara 2,3,4,5 na kujikuta wakiambulia wanaume/wanawake wale wale wasio sahihi
kwake.
Mwanamnke mmoja aliyejitambulisha
kwa jina la Suzzy aliwahi kuniomba ushauri, akasema amechoka kuchezewa, maana
kila mwanaume anayempata anakuwa si chaguo lake. Lakini kibaya zaidi kuachia
ngazi au kutemwa huku akiwa tayari ameshafanya mapenzi na wanaume hao.
Nia ya swali lake ilikuwa ni
kuniomba njia za kumtambua mwanaume mkweli bila kufanya naye mapenzi? Aliuliza
hivyo huku akiwa na hoja kuwa wanaume wengi hawako tayari kuwa na uhusiano na
msichana bila kufanya naye mapenzi na wakati huo huo huficha tabia zao chafu
wakilenga kumnasa wamtakaye.
Binafsi nafahamu kuwa kuna
wanawake/wanawake wengi ambao hujiingiza katika mapenzi kwa kutekwa na hadaa za
mwili na kujikuta wanacheza mchezo wa kitoto wa pata potea.
Ni madhumuni ya somo hili
kufundisha vigezo vya kumpata mwanaume/mwanamke halisi wa maisha, bila kufanya
naye mapenzi. Njia hii ina faida kwa pande zote mbili yaani kwa mwanamke na
mwanaume kwani kuacha au kuachwa bila kufanya mapenzi ni bora kuliko kuwa
muonjaji, tabia ambayo huathiri kisaikolojia na ni hatari kwa afya.
Ifuatavyo ni njia ya kisaikolojia
ambayo mwanamke anaweza kutumia kumpata mwanaume mwenye kumfaa bila kufanya
naye mapenzi tena ni jibu sahihi la kuondokana na mchezo wa kubahatisha kwa
wanaume wanaosaka wapenzi wa kweli na si taksi bubu ambazo mchana huweka namba
za njano usiku nyeusi.
KWANZA- Ni ya mwanamke/mwanaume
mwenyewe kujifahamu na kufahamu vigezo vya mpenzi anayemhitaji katika maisha
yake. Ifahamike kuwa kila mwanaume ana wake na kila mwanamke anaye wake wa
maisha pia. Hivyo asiyekufaa wewe anawafaa wengine, kinachotakiwa ni wewe
kujitambua kwanza ili umtambue umtakaye.
Wanawake/wanaume wengi hawafahamu
wanahitaji wapenzi wa aina gani, hivyo wanajikuta kama watu wanaoingia sokoni
bila kujua wanataka kununua nini? Ndiyo maana wengi wameangukia kwa matapeli wa
mapenzi, wakachezewe na kuumizwa moyo bure.
PILI- Ni kuketi chini na
kuorodhesha vigezo stahili vya mwanaume/mwanamke unayemtaka. Baada ya hapo
orodhesha tena kasoro za mwanaume/mwanamke unazoweza kuzivumilia na zile ambazo
huwezi kuzivumilia kabisa. Hii inatokana na ukweli kwamba mwanadamu
hajakamilika, ana upungufu wake.
TATU- Anza kumsaka kwa kutumia
milango ya fahamu. Cha kufanya hapa ni kuruhusu macho yawaone wanaume/wanawake
na kuwatathmini kwa maumbile yao ya nje na kisha kupata majibu kutoka moyoni
juu ya kuvutia kwao ambako hutambulika kwa moyo kurithika na mwili kusisimka.
NNE - Kuanzisha safari ya
kuchunguza tabia za nje na za ndani kivitendo. Hapa suala la ukaribu baina ya
mwanaume na mwanamke linahitajika. Msingi unaotajwa hapa ni kujenga mazoea ya
kawaida yasiyokuwa na masuala ya kimapenzi na ngono. Kutambuana, dini, viwango
vya elimu, kabila na makundi ya marafiki ni mambo ya kuzingatia.
Katika uchunguzi huu
mwanamke/mwanaume anayetafuta mpenzi hana budi kupitia na kumlinganisha huyo
aliyempata na vigezo alivyojiwekea. Zoezi hili liendane na kuweka alama ya pata
kila anapobaini kuwa mwanaume/mwanamke anayemchunguza amepata moja ya vigezo
vyake. Lakini pia aweke alama ya kosa kwa kila kasoro anayoivumilia na ile
asiyoivumilia.
TANO - Ajipe muda wa kutosha kati
ya miezi sita na mwaka kumchunguza huyo mwanaume, kisha aketi chini na aanze
kujumlisha alama za vigezo alivyovijiwekea na jinsi mwanaume huyo alivyopata au
kukosa.
Ikibainika mwanaume
aliyechaguliwa amepata zaidi ya nusu ya alama ya vigezo vilivyowekwa, basi ujue
kuwa anafaa. Kuhusu alama chache alizikosa anaweza kusaidia kuzikamilisha
polepole wakati wa maisha ya ndoa.
Lakini angalizo kubwa kabisa ni
kwamba mwanaume/mwanamke akionekana kuanguka katika kasoro zisizoweza kuvumilia
kwa zaidi ya alama tatu. Yaani kwa mfano ni mlevi, mwizi, muongo, mbishi na
katika hizo kashindwa 3, huyu hafai, ni vema akawekwa kando kwani huwezi kubeba
kero 3 kwa pamoja katika maisha.
SITA - Kusajili mapenzi yenye
malengo yanayotekelezeka. Lazima baada ya kuchunguzana kwa kina wapenzi
watengeneze muongozo wa mapenzi yao. Wasiwe kama wanyama, lazima mipango ya
wapi wametoka walipo na wanapokwenda.
Hata hivyo watalaam wanasema
lazima wapenzi wapime umakini wao kwa vitendo. Kama wamekubaliana kuoana, suala
la mume kwenda kujitambulisha kwa wakwe na hatua ya kuiendea ndoa ionekane.
Usiri usiwepo tena. Kila mmoja amuone mwenzake kama sehemu ya maisha yake na
mara zote wasaidiane kwa ukaribu.
SABA - Ni vema ndugu
wakashirikishwa ili kuwapa nafasi na wao ya kuamua kama mapenzi hayo ni budi
yakaendelea au yakasitishwa. Ni ukweli ulio wazi kwamba licha ya wengi kupuuza
maamuzi ya ndugu kwa madai ya kuwa hawana nafasi kwa wapenda nao, lakini
uchunguzi unaonesha kuwa wapenzi wengi huacha kutokana na sumu za ndugu hasa
pale wanapokuwa wameonesha kutounga mkono uhusiano wa wanaotaka kuoana
NANE - Hatua hii ni ya kuweza
kuzungumzia ufanyaji mapenzi, hapa nina maana kama wapenzi wamejizuia kwa muda
mrefu na wanahisi kuchoka wanaweza kujadiliana kuhusu hilo na kuamua ufanyaji
huo wa mapenzi una lengo gani, kama ni kuburudisha miili basi suala la afya na
uzazi salama litazamwe.
TISA - Kutimizwa kwa ahadi ya
kuoana ni hatua ya tisa ambayo nayo si busara ikachukua muda mwingi
kutekelezeka, kwani ucheleweshaji mwingi wa ndoa nao huvunja moyo na mara
nyingine umewafanya wengi kutoaminiana.
KUMI - Kuamua kuwa mwili mmoja
kwa kuvumilia na kuwa tayari kukabiliana na changamoto zote za maisha ukiwemo
mkwamo na dhiki ambazo huchangia sana ndoa nyingi kuvunjika. Hapa pia ni wajibu
wa wanandoa kuchukuliana udhaifu na kusaidia, kuwa tayari kujifunza na kujali
zaidi upendo kuliko hisia za mwili ambazo wakati mwingine hudanganya na hivyo
kumfanya mwanandoa asivutiwe na mwenzake.
Mwisho ni kwamba kanuni hizi
huwafaa watu wazima mapenzi ya kitoto hayawezi kujenga misingi hii imara mara
nyingi ni kudanganyana, kuharibiana maisha, kupeana mimba na maradhi.
Karibu tuendelee kuelimishana
JEROME MMASSY
JESAM BLOGSPOT

No comments:
Post a Comment