Monday, 21 March 2016

WANAFUNZI WANAJISIWA MOSHI: NI MAAJABU YA KARNE YA 21

Watoto wanne wa kike wenye umri wa miaka nane, wamebainika kubakwa na kunajisiwa kwa karibu mwaka mmoja huku vijana wawili wanaowafanyia vitendo hivyo wakiwalipa Sh500 kila mmoja.

Habari zinasema watoto hao wanaosoma darasa la tatu katika shule ya msingi ya Msaranga katika Manispaa ya Moshi, wamekuwa wakienda kufanyiwa vitendo asubuhi kabla ya kuingia darasani.

Uchunguzi wa madaktari wa hospitali ya rufaa ya mkoa Kilimanjaro ya Mawenzi umethibitisha watoto hao kuingiliwa sehemu za siri na kunajisiwa na pia wameambukizwa magonjwa ya zinaa.

Watoto hao wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo kati ya saa 12:30 na saa 1:30 asubuhi na baadae hutakiwa kurudi saa 4:00 wakati wa mapumziko ili kuchukua Sh500 kama malipo ya kazi hiyo.

Tukio hilo ambalo limeibua hasira za wananchi, linafanana kwa kiasi na lile la mwanamuziki Nguza Viking “Babu Seya” na mwanae Jonson Nguza “Papii Kocha” wanaotumikia kifungo cha maisha jela.

Wanamuziki hao raia wa Congo walihukumiwa kifungo hicho mwaka 2004 kwa tuhuma za kubaka na kunajisi watoto 10 wenye umri wa miaka 6 na 8 wa shule ya msingi Mashujaa ya Jijini Dar Es Salaam.

Mzee Alex Massawe (sio jina lake halisi), mkazi wa Msaranga mjini Moshi, alisema kuwa Jumatano iliyopita, alishuku mwenendo usio wa kawaida wa mjuu wake mwenye umri wa miaka nane.

“Ilikuwa kwenye saa 12:30 au saa 1:00 asubuhi nilikuwa natoka misa ya asubuhi nikakutana naye anavuka na wenzake wanavuka barabara kwenda upande tofauti na ilipo shule,”alisema mzee huyo.

“Nilipomuuliza unaenda wapi akasema mwalimu amewatuma madekio lakini nikamuona anatetemeka. Nikamwamuru arudi shule mara moja. Mie nikaendelea na safari yangu lakini roho inakataa”.

Mzee huyo anasema saa 2:00 asubuhi siku hiyo hiyo akarudi shuleni kwa lengo la kukutana na mwalimu mkuu lakini akakutana na mwalimu wa zamu na kumweleza mashaka yake.

Kwa mujibu wa mzee huyo, mwalimu wa zamu aliahidi kuchunguza jambo hilo, lakini siku hiyo mjukuu wake aliporudi nyumbani alimuuliza na baada ya kumchapa kidogo akaeleza kila kitu.

Siku iliyofuata mzee huyo akarudi shuleni na kumweleza mwalimu mkuu taarifa zile ambaye aliita walimu wenzake na kumwita mtoto huyo na kumuuliza kama ni kweli alichoeleza babu yake.

“Mwalimu mkuu akamwambia usiposema ukweli nitakuadhibu ndio akasema kuna wavulana fulani wanaendaga kwao kufanya hayo mambo na akawataja wenzake watatu ambao huendaga nao,”alisema.

Mlezi huyo alidai mbele ya walimu alieleza kuwa huwa wanakwenda huko asubuhi na kufanyiwa ufirauni huo kwa zamu katika chumba kimoja halafu hutakiwa kurudi saa 4:00 kuchukua Sh500.

“watoto wawili akiwemo huyu mjukuu wangu walikiri na kuwataja kwa majina hao vijana na kutueleza fulani huwa anatufanya mbele na fulani anatufanya nyuma. Wawili waligoma kueleza,”alisema.

“Wakatuambia saa 4:00 wakati wa break (mapumziko) ndio wanaenda kuchukua hiyo mia tano mia tano halafu siku zingine hurudi saa 8:00 mchana kufanya mambo hayo kadri wanavyokubaliana”.

“Hivi tunavyoongea nimekosa usingizi siku zote hizi. Sina amani moyoni. Najiuliza maswali mengi ambayo nakosa majibu. Kwanini ushetani huu kwa watoto wadogo kama hawa?”alihoji mzee huyo.

Mtoto huyo alipoulizwa, alieleza maelezo yanayofanana na ya babu yake na kuwataja kwa majina vijana hao, mmoja jina lake likianzia na herufi J na mwingine jina lake likianzia na herufi W.

Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mtafungwa, alilithibitishia kuwapo kwa tukio hilo na kueleza kuwa tayari polisi wamemtia mbaroni mtuhumiwa mmoja wa tukio hilo.

“Ni kweli kuna shauri hilo limefunguliwa na tayari tumemkamata mmoja wa watuhumiwa na tunaendelea kumtafuta mwingine anayetajwa na watoto hao,”alisema Kamanda Mtafungwa.

No comments:

Post a Comment

Featured post

MWANAMKE YAFUATE HAYA; NI MUHIMU KWA MAHUSIANO YAKO

1. Degree yako ya fist class uliyoipata chuo kikuu haiwezi kukufanya uwe mke first class katika ndoa yako bali ni heshima yako na uthubu...