Saturday, 5 March 2016

WALIMU MWANZA MBARONI KWA UBAKAJI


MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo jana aliamuru kukamatwa kwa walimu wanane wa Shule ya Sekondari Mihama katika Manispaa ya Ilemela kwa kosa la kukiuka maadili ya utumishi wa umma, kwa kutuhumiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na baadhi ya wanafunzi wa kike wa shule hiyo.
Akizungumza shuleni hapo, Mkuu huyo wa mkoa alisema walimu hao wamedhalilisha taaluma ya ualimu kwa vitendo vyao hivyo.
Mulongo aliongozana na Ofisa Elimu wa mkoa wa Mwanza, Hamis Maulidi, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Manju Msambya na Mkuu wa Takukuru wilaya ya Ilemela, Debora Mlowe na Katibu wa Chama cha Walimu Mkoa wa Mwanza(CWT), Said Selemu na Kamati ya Ulinzi na usalama ya wilaya ya Ilemela.
Kati ya walimu hao wanane, ni walimu watano ndio walikamatwa jana majira ya saa kumi na kuwekwa chini ya ulinzi na polisi, ambapo walifungwa pingu na kupandishwa ndani ya gari la polisi.

Waliokamatwa na kuwekwa rumande ni Mkuu wa Shule hiyo, Joseph Malifedha, ambapo Mkuu wa Mkoa alimuagiza Katibu wa Idara ya Utumishi wa Walimu mkoa wa Mwanza, Genzi Sahani kumvua madaraka yake ya ukuu wa shule mara moja.
Wengine ni Rodrick Urock, Denis Sanga, Edmund Boaz, Steven Samwel, aidha alimuagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Ilemela, Sweetbert Kisha kuwasiliana na polisi mkoani Tanga ili kuhakikisha kuwa mwalimu Abdallah Mweve aliyehamishiwa mkoani humo ambaye pia amehusishwa na tuhuma hizo anakamatwa mara moja na kurudishwa mkoani Mwanza.
Mulongo aliagiza pia kuwakamata walimu wawili, Yoeza Mzava na Joseph Ramongi waliohamishiwa katika Shule ya Msingi Sangabuye, ambao nao wanatuhumiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi, jambo ambalo alisema ni la aibu kwa watumishi wa umma.
Alisema awali alifika shuleni hapo Januari 27 mwaka huu katika ziara yake ya kikazi na kupokea malalamiko hayo kutoka kwa wazazi na walezi wa wanafunzi hao, hali iliyomfanya kuunda tume mara moja kushughulikia tatizo hilo.
“Hili ni jambo la hovyo kabisa, walimu kwa mujibu wa Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 kufanya mapenzi na wanafunzi ni kosa la jinai, hawa wote wawekwe chini ya ulinzi na ikithibitika wafikishwe mahakamani mara moja.”
Wakati huo huo, Mkuu huyo wa Mkoa alimuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Shule kuvunja mara moja bodi ya shule hiyo kwa sababu tangu iteuliwe mwaka 2013 haikuwahi kuitisha vikao vya shule, jambo lililofanya shule hiyo kutoitisha vikao vya bodi ambavyo ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya shule.

No comments:

Post a Comment

Featured post

MWANAMKE YAFUATE HAYA; NI MUHIMU KWA MAHUSIANO YAKO

1. Degree yako ya fist class uliyoipata chuo kikuu haiwezi kukufanya uwe mke first class katika ndoa yako bali ni heshima yako na uthubu...