Thursday, 25 February 2016

Njia Bora Ya Wewe Kuweza Kufikia Malengo Na Mipango Yako Mikubwa Kwenye Maisha Yako.


Habari za wakati huu msomaji wangu? Nina imani kwamba uko vyema na unaendelea vizuri kuweka ubora kwenye kila unachofanya maishani mwako. Hili ni jambo muhimu sana kwani ndio litafanya maisha yako yawe bora na wewe uweze kuyafurahia. 

Katika maisha yetu, kuweka malengo na mipango ni hatua moja muhimu sana ya wewe kuanza safari ya kuboresha maisha yako. lakini kuweka tu malengo na mipango sio jawabu la maisha bora kwako. Ingekuwa hivi kila mtu unayekutana naye angekuwa na maisha bora sana. Hii ni kwa sababu kila mtu ana mipango mizuri sana na maisha yake.
 
Eneo muhimu sana litakalobadili maisha yako ni kuweza kufanyia kazi malengo na mipango yako. kuweza kukomaa nayo hata pale unapokutana na changamoto, na kwa hakika ni lazima utakutana na changamoto


Wengi hawafiki mbali. 

Kwa mfano tuanze na mwanzo wowote wa mwaka. Watu wengi hufurahia mwaka mpya, huweka malengo ya mwaka huo na kuwa na mategemeo makubwa sana. Lakini kadiri siku zinavyokwenda ile hamasa inaanza kupungua na baada ya muda wengi wanakuwa wameachana kabisa na yale malengo na mipango yao. Inapofika tena mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka unaofuatia zoezi hili linaanza tena. 

Watu wengi wamekuwa wakirudia hivi miaka nenda miaka rudi, je na wewe ni mmoja wao? Je leo ukipata njia ya uhakika ya kukuwezesha wewe kufanyia kazi malengo na mipango yako utaifanyia kazi? Kama ndiyo basi endelea kusoma. 

Kushindwa ni kukubwa kuliko kushinda.

Watu wengi hivi kuishia njiani licha ya kujiwekea malengo na mipango mizuri haitokei tu kwa sababu imetokea, kuna sababu kubwa sana ambazo zipo nyuma ya hili. Sitaki kukukatisha tamaa lakini ninachoweza kukuambia ni kwamba kwa jambo lolote unalofanya au unalotaka kufanya, uwezekano wa kushindwa au kukata tamaa ni mkubwa kuliko ule wa kushinda. 

Kushindwa ni kukubwa kwa sababu kila jambo kubwa ambalo unakwenda kufanya linakuwa na changamoto zake ambazo hujawahi kuzijua hapo kabla. Na hivyo unapokutana nazo ni rahisi sana kuamua kuacha kuendelea. 

Sababu nyingine inayopelekea kushindwa iwe rahisi ni wale wanaokuzunguka, unaweza kukazana na kuzivuka changamoto, ila sasa ukakutana na nguvu ya kupinga kutoka kwa wale watu ambao wanakuzunguka. Watu ambao ni wa karibu kwako na wanakujua vizuri. Watu hawa wanakuletea habari za kukukatisha tamaa kwamba utashindwa, au huwezi au unachofanya hakitafanikiwa. Na wakati mwingine watakuletea mpaka na mifano ya watu ambao walijaribu kama wewe na wakashindwa. 
Kwa vikwazo hivi ni rahisi sana kuamua kuachana na kile ulichopanga na kuamua kurudia maisha yako ya kawaida. 

Kuna mtu anaweza kukusaidia kuvuka vikwazo hivyo. 

Kama huwa unafuatilia mchezo wowote, hasa mpira wa miguu utagundua kwa mfano, Ronaldo au Messi ni wachezaji wenye uwezo mkubwa sana. Lakini wachezaji hawa hawajiendei tu wenyewe jinsi wanavyotaka, japo wanaweza kujiwekea mipango yao wao wenyewe. Bali wachezaji hawa bora sana wana makocha wao ambao wanawasimamia vyema kwenye malengo na mipango yao ya kutaka kuwa wachezaji bora zaidi. 
Mchezo wowote kuna mtu ambaye ni kocha, mtu huyu anakuwa na jukumu la kuifundisha na kuiongoza timu ili iweze kufanya vizuri na kufikia malengo ambayo kila mmoja amejiwekea. 

Kocha hataingia uwanjani kucheza, lakini kocha anazijua mbinu bora sana ambazo kama wachezaji wake watazitumia basi wataweza kushinda mashindani wanayoshiriki. Kocha anao uwezo wa kuona changamoto na suluhisho la changamoto hizo zaidi ya mchezaji ambaye yuko uwanjani anacheza. 
Timu zote ambazo zimefanya vizuri, wachezaji wote ambao wamefanya vizuri ni kwa sababu wamekuwa na makocha wazuri. 

Mshirikishe mwingine aendelee kunifuatilia kupitia Blog hii ili tushirikishane mambo mengi ya msingi.

Itaendelea katika toleo lingine!!


No comments:

Post a Comment

Featured post

MWANAMKE YAFUATE HAYA; NI MUHIMU KWA MAHUSIANO YAKO

1. Degree yako ya fist class uliyoipata chuo kikuu haiwezi kukufanya uwe mke first class katika ndoa yako bali ni heshima yako na uthubu...