Siku chache baada ya Mhe.John Pombe Magufuli kuchaguliwa kuwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuanza "kutumbua majipu"
rafiki yangu mmoja ambaye ni mwandishi wa gazeti moja la kila siku aliniambia
hii ni nguvu ya soda.
Alisema Magufuli anaweza kuwa na dhamiri ya kweli ya kufanya
mabadiliko lakini atakwamishwa na chama chake. Ba
do chama chake hakijawa na
dhamira ya kweli ya kutaka mabadiliko. Hata majipu anayotumbua kuna mengine
hayatumbuliki maana yanagusa uhai wa chama chake.
Aliifananisha dhana ya "kutumbua majipu" na
"kuvua gamba" ambayo ilitumika na chama cha mapinduzi miaka kadhaa
iliyopita kama ajenda ya kupiga vita ufisadi. Lakini ajenda hii ilishindwa
kuvua hata gamba moja ndani ya chama hicho licha ya kupigiwa chapuo na viongozi
wakuu wa chama hicho.
Kwahiyo dhana ya "utumbuaji wa majipu" ni sawa na
"uvuaji gamba". Kuna majipu hayawezi kutumbulika hata kama Rais
Magufuli ana dhamira ya kufanya hivyo.
Moja ya jipu kubwa kabisa ambalo lipo usoni kwa Magufuli na
amelikalia kimya kama hajaliona ni suala la umeya wa Jiji la Dar es Salaam.
Hili ni jipu ambalo Magufuli ameshindwa kulitumbua na haoneshi kuwa na mpango
huo.
Tangu uchaguzi mkuu ufanyike na wananchi kuchagua wabunge na
madiwani yapata miezi minne sasa. Katika kipindi hiki cha miezi minne jiji la
Dar es salaam ni kama limesimama.
Jiji halina Meya, hakuna kamati za halmashauri, hakuna mipango
ya maendeleo, hakuna vikao vya madiwani, jiji limesimama kwa sababu ya mvutano
wa kisiasa kati ya CCM na Muungano wa vyama vya UKAWA juu ya nafasi ya Umeya.
Mvutano huu umesababishwa na CCM kutokubali kuachia madaraka
ya kuongoza jiji la Dar kwa vyama vya upinzani. Bado haijajulikana hofu ya CCM
inatokana na nini lakini hadi sasa wamefanya mbinu mbalimbali kuhakikisha
wanahujumu uchaguzi wa Umeya wa Dar na kuweza kuongoza tena jiji hili.
Baadhi ya mbinu zilizotumika ni pamoja na kutumia wabunge wa
viti maalumu kutoka Zanzibar ambao baada ya mvutano mkubwa wa kisheria
walizuiwa kupiga kura ya kumchagua Meya.
Lakini watu wanahoji kwanini CCM walete wabunge wa Zanzibar
kuja kupiga kura Dar? CCM walijua kuwa wabunge wa Zanzibar hawana uhalali wa
kisheria wa kupiga kura bara lakini wakalazimisha. Kwanini?
Baada ya wabunge hao kuzuiwa kushiriki uchaguzi huo CCM
hawakuridhika. Wakabuni mbinu nyingine ya kuwatumia Mawaziri walioteuliwa kuwa
wabunge kabla ya kuapishwa. Hilo nalo likakumbana na kizingiti cha kisheria.
Hatimaye uchaguzi ukaitishwa tena tarehe 05 mwezi February
mwaka 2016 lakini Chama cha mapinduzi kikakimbilia Mahakamani kuweka zuio la
kuahirisha uchaguzi huo. Kwahiyo wajumbe wakafika ukumbini na kutangaziwa kuwa
uchaguzi huo umeahirishwa.
Hatimaye uchaguzi huo ukaitishwa tena kwa mara ya nne jumamosi
ya tarehe 27 mwezi February mwaka huu.
Katika uchaguzo huo Theresia Mbando aliyekuwa Mwenyekiti wa
Mkutano huo, aliwataka wajumbe wote kuingia ukimbini ili mkutano huo kuanza.
Baada ya wajumbe kuingia ndani, Mbando alifuata taratibu zote
za kiitifaki katika kufungua kikao hicho ikiwa ni pamoja na kugawa ratiba za
mkutano huo.
Wajumbe wakiwa tayari kwenda na ratiba ya mkutano huo, ndipo
Bi.Sara Yohana (Kaimu Mkurugenzi wa jiji) alisimama ghafla na kutangaza
kuhairishwa kikao hicho kwa madai kwamba, amepokea zuio kutoka Mahakama ya
Kisutu iliyomtaka kutoendesha uchaguzi huo. Hali hiyo ilizua taharuki na
kusababisha vurugu kubwa.
Katika maelezo yake kwa wajumbe Bi.Sarah alionesha nakala ya
zuio la Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu iliyotolewa tarehe 5 mwezi February
mwaka huu.
Watu wanahoji ikiwa kulikua na zuio la Mahakama kuanzia tarehe
5, kwanini Mkurugenzi aliitisha uchaguzi na kualika wajumbe? Kulikua na haja
gani ya kujulisha umma kuwa uchaguzi upo na watu wakafika kumbe kuna zuio la
mahakama?
CCM WANA HOFU GANI?
Kutokana na hali inayoendelea yapo maswali mengi yanayoibuka juu ya hofu ya CCM
kwenye uchaguzi huu. Je kwanini CCM hawataki kuachia Halmashauri ya jiji
iongozwe na upinzani? Wanahofia nini?
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema CCM wana
hofu mbili. Kwanza wanahofia kupoteza mamlaka ya kimaamuzi katika mambo
yanayohusu maendeleo ya jiji la Dar.
Kwa kuwa jiji litaongozwa na upinzani, CCM watakosa nguvu ya
kufanya maamuzi katika mipango ya maendeleo ya jiji, na hivyo watashindwa
kutekeleza ilani yao. Hali hii itatoa fursa kwa vyama vya UKAWA kutumia nafasi
hii kujiimarisha zaidi kimipango, mikakati na kuwa na mamlaka kuzidi CCM.
Ikumbukwe halmashauri ya jiji la Dar es Salaam ndiyo
inayoongoza kwa makusanyo ya mapato kulinganisha na Halmashauri nyingine
nchini. Halmashauri ya jiji la Dar inakadiriwa kukusanya jumla ya shilingi
Bilioni 10.7 kwa mwezi, ambapo kati ya hizo Bil 6.9 ni mapato ya ndani na Bil
3.8 ni ruzuku ya serilali. Mapato haya ni makubwa kuliko maapato ya majiji yote
yaliyosalia ukiyaweka kwa pamoja.
Pengine hii ndiyo hofu ya CCM. Kwamba wanahofia fedha hizi
zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo chini ya utawala wa vyama vya
upinzani na hivyo vyama hivi vitapata fursa ya kujiimarisha zaidi.
Lakini upo mtizamo mwingine kwamba hofu ya CCM sio juu ya
yatakayofanyika bali juu ya yaliyofanyika. Hawahofii UKAWA watafanya nini
wakiingia madarakani, wanahofia wao walifanya nini walipokua madarakani.
Kuna taarifa kuwa kuna uchafu mwingi katika Halmashauri ya
jiji la Dar na CCM wanahofia UKAWA wakishinda uchaguzi wataweka wazi uchafu
huo.
Yapo madai kuwa miradi mingi ya maendeleo ilitekelezwa chini
ya kiwango kwa kuwa wakandarasi walilipwa pesa kidogo kulinganisha na bajeti
iliyotengwa. Pesa nyingine zilifanyiwa ufujaji na watendaji wa halmashauri.
Hivyo CCM wanahofia ikiwa UKAWA wataingia madarakani watawaumbua.
Mojawapo ya miradi yenue malalamiko mengi ni uuzwaji wa
Shirika la la Usafiri Dar es Salaam (UDA) amabalo liliuzwa katika mazingira ya
kutatanisha kwa kampuni ya Simon Group ya jijini Mwanza.
Tarehe Mei 24, 2011 Mkurugenzi mkuu wa Simon Group Ndugu Simon
Kisena alimuandikia barua Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu akimjulisha kuwa
hadi wakati huo yeye ndiye aliyekuwa mmiliki mkuu wa UDA, baada ya kununua hisa
7,880,303 sawa na asilimia 52.35 ya hisa zote za UDA kati ya hisa 15,000,000 za
awali kwa gharama ya Sh milioni 285.
Lakini gazeti la Jamhuri la tarehe 26 January mwaka 2016
liliandika habari juu ya ukaguzi uliofanywa kwenye kampuni hiyo ya Simon group
na kampuni ya ukaguzi ya Philip & Company ilionesha kuwa Kampuni ya Simon
Group ilipata faida ya Bilioni 1.7 baada ya kufanya kazi mwezi mmoja tu tangu
walipoinunua UDA.
Yani walinunua UDA kwa Milioni 285 lakini baada ya kufanya
kazi kwa mwezi mmoja tu wakapata faida ya Bilioni 1.7. Hii ni faida kubwa sana
na isiyotarajiwa katika mazingira ya kawaida.
Ikiwa UDA ilikua na uwezo wa kuingiza faida ya Bilioni 1.7 kwa
mwezi kwanini iliuzwa kwa Milioni 285 tu? Bila shaka kuna mazingira ya ufisadi
katika sakata la uuzwaji wa UDA. Wapo viongozi kadhaa ambao wamewahi kutuhumiwa
kuwa walishiriki kuuza UDA kinyemela.
Huu ni mfano mmoja tu kati ya mifano mingi inayohusu uchafu
uliofanyika katika halmashauri ya jiji la Dar wakati jiji likiongozwa na CCM.
Na pengine uchafu wa aina hii ndio unaowapa hofu CCM kuachia halmashauri hii
kuongozwa na vyama vya upinzani kwa vile wataumbuka.
Kama wameweza kuumbuka Ilala sembuse halmashauri ya jiji?
Taarifa ya Meya wa Ilala Mhe.Charless Kwiyeko aliyoitoa mwishoni mwa wiki
iliyopita inaonesha kuwa kuna ubadhirifu mkubwa ulifanyika katika halmashauri
hiyo wakati ikiwa inaongozwa na CCM.
Mojawapo ni mishahara kwa mgambo wa jiji. Taarifa ya ukaguzi
ilionesha kuwa Askari Mgambo wa jiji hulipwa kiasi cha shilingi 280,000/= kwa
mwezi lakini malipo halisi waliyokua wakipata ni shilingi 60,000/= kwa mwezi.
Hii ina maana kwamba kila Askari Mgambo alikua akikatwa
shilingi 220,0000/= katika mshahara wake ambapo alikua hajui zinapoenda. Huu ni
ufisadi na unyonyaji wa kiwango kisichovumilika.
CCM WANA MPANGO GANI?
Hadi sasa CCM wametumia mbinu mbalimbali kuhakikisha wanaongoza halmashauri ya
jiji la Dar lakini imeshindikana. Pamoja na kutumia madiwani kutoka Zanzibar na
kuweka zuio mahakamani bado wana hofu ya kushindwa uchaguzi kwa kuwa wana idadi
ndogo ya madiwani kulingamisha na wale wa UKAWA. CCM ina jumla ya madiwani 76
na UKAWA 87 hivyo inatarajiwa Uchaguzi ikifanyika CCM wataanguka.
Lakini pamoja na kuwa na idadi ndogo ya madiwani bado wana
mpango wa kuongoza halmashauri ya jiji la Dar kwa kutumia mbinu yoyote. Kwa
kuwa demokrasia inaonekana kushindwa kuwapa fursa ya kuongoza wanaweza kutumia
mbinu nyingine zisizo za kidemokrasia.
Mbinu kubwa inayotarajiwa ni kama ile iliyotumika mwaka 1996.
Tarehe 28 mwezi June mwaka 1996 aliyekuwa Waziri Mkuu Mhe.Fredrick Sumaye
aliivunja Halmashauri ya jiji la Dar na kuunda Tume maalumu ya muda kwa ajili
ya kuongoza jiji hilo kwa madai ya rushwa na jiji kukusanya mapato chini ya
kiwango.
Sheria ya serikali za mitaa ya mwaka 1982 [Local Government
Act (Urban Authorities) of 1982] pamoja na sheria nyinginezo zinazosimamia
serikali za mitaa na majiji zinampa Waziri Mkuu mamlaka ya kuvunja halmashauri
ya jiji/mji/manispaa na kuteua Tume ya muda ya kuongoza eneo hilo.
Lakini ili kufanya hivyo ni lazima kuwepo na sababu ya
kumfanya Waziri Mkuu kufanya maamuzi hayo. Mwaka 1996 Sumaye aliivunja
halmashauri ya jiji kwa kuwa alikua na sababu. Hakuivunja tu kienyeji. Na sabu
zenyewe ni mbili. Moja ni madai ya rushwa na pili ni kukusanya mapato chini ya
kiwango.
Lakini mwaka huu Waziri Mkuu hana sababu ya kumfanya aamue
hivyo. Kama ni mapato, jiji la Dar wanakusanya zaidi ya matarajio. Mwaka
2014/15 walipanga kukusanya Bilioni 10.1 kwa mwaka lakini wakakusanya wastani
wa Bilioni 10.7 (zidio la milioni 600).
Kwa hiyo Waziri Mkuu hana sababu ya kuivunja Halmashauri ya
jiji lakini CCM wanataka kumpa sababu.
Kitendo cha kuitisha uchaguzi huku wakijua wazi kwamba kuna
zuio la Mahakama inaonekana ni mpango wa kuwakasirisha wafuasi wa UKAWA
waliokua wamefurika ukumbini ili wafanye fujo na Waziri mkuu atumie fujo hizo
kama kigezo cha kuvunja halmashauri ya jiji na kuunda Tume ya muda kuongoza.
Kwa kufanya hivyo atakua amefanikiwa kuhujumu haki ya UKAWA
kuongoza jiji la Dar na kuwapa fursa CCM kubaki madarakani kupitia mlango wa
uani wa kuunda Tume.
RAIS MAGUFULI ANA NAFASI GANI KATIKA HILI?
Watu wengi wanajiuliza kwanini Rais Magufuli amekaa kimya juu ya suala hili kwa
takribani miezi minne sasa. Magufuli ambaye amejitanabaisha kuwa muadilifu
kwanini hachukui hatua zozote juu ya swala hili. Kitendo cha kukaa kimya huku
akishuhudia demokrasia ikibakwa kinatilia mashaka uadilifu wake.
Hali hii inafanya watu wafike mbali zaidi na kuhoji juu ya
ushindi wake. Ikiwa CCM hawako tayari kushindwa katika ngazi ya halmashauri ya
jiji, je wangeshindwa katika uchaguzi mkuu nafasi ya Rais wangekubali.?
Ikiwa jambo dogo kama la umeya wamekataa kuheshimu demokrasia,
je wanaweza kuheshimu demokrasia katika Uchaguzi ngazi ya kitaifa?
Kwanini Rais Magufuli anatumbua majipu yaliyojificha lakini
jipu la Umeya Dar analilea? Kwanini asiwashauri CCM waheshimu demokrasia na
maamuzi ya Wananchi?
Miezi minne sasa jiji la Dar es Salaam limesimama. Hakuna
mipango ya maendeleo, hakuna vikao vya halmashauri kwa sababu ya CCM kukataa
kuheshimu demokrasia. Je Magufuli anaona hili ni sawa?
Kwamba watu waendelee kuteseka kwa kukosa huduma, mipango ya
maendeleo isipangwe, kwa sababu tu CCM hawako tayari kushindwa? Je hii ni sawa?
Kitendo cha Rais Magufuli kukaa kimya kwenye suala hili
kinamfanya aonekane hana dhamira ya kweli ya kuleta mabadiliko. Hana tofauti na
watangulizi wake. Anakipenda zaidi chama chake kuliko anavyowapenda watanzania.
Ndio maana yuko tayari kuona chama chake kikivunja demokrasia na wananchi
wakiteseka lakini akakaa kimya, kwa sababu tu uvunjaji huo wa demokrasia
unakinufaisha chama chake.
Hili ni doa katika utendaji wake, na asipochukua hatua za
dharura atapoteza imani yake aliyoanza kuijenga mbele ya jamii ya Watanzania.
Malisa GJ.!

No comments:
Post a Comment